JOWUTA ,IFJNA THRDC WAJIPANGA KUNOA WAANDISHI WA HABARI KURIPOTI UCHAGUZI !

 JOWUTA,IFJ na THRDC kutoa mafunzo ya kuripoti uchaguzi mkuu.

Ngilisho Tv,Dar es Salaam.


Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari nchini(JOWUTA) kwa kushirikiana na shirikisho la kimataifa la waandishi duniani(IFJ) na Mtandao wa watetezi wa haki za binaadamu(THRDC) wanatarajia kuanzia mwezi huu  kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini jinsi ya kuripoti uchaguzi mkuu wakiwa salama.


Mafunzo hayo ambayo yanaratibiwa na JOWUTA katika awamu ya kwanza yanatarajiwa kufanyika katika kanda tatu nchini, ambazo ni Kanda ya Pwani ,Kanda ya Nyanda za juu kusini na Kanda ya Kaskazini ambayo itaandamana na maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uhuru wa habari ambayo itafanyika jijini Arusha.


Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma ametoa taarifa hiyo leo April 10,2025 baada ya viongozi wa JOWUTA kutembelea makao makuu ya ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binaadamu(THRDC) jijini Dar es salaam, kufanya mazungumzo na Mratibu wa kutaifa wa mtandao huo, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa.


Juma alisema katika mkutano wa waandishi wa habari Afrika uliofanyika nchini Senegal na baadae Rwanda, aliomba IFJ na shirikisho la waandishi Afrika(FAJ) kusaidia mafunzo kwa wanahabari Tanzania ili waweze kuripoti uchaguzi kwa haki na salama.


"Niliomba watusaidie mafunzo na baada ya majadiliano baina yao IFJ ikakubali kugharamia sehemu ya mafunzo "alisema


Hata hivyo alisema kutokana na mafunzo kuhitaji gharama kubwa JOWUTA iliamua kuanza kutafuta wadau wengine kushirikiana nao wakiwepo THRDC.





Akizungumza baada ya maelezo hayo, Wakili Onesmo Ole Ngurumwa alisema THRDC itachangia sehemu ya gharama za kufanikisha mafunzo kwa wanahabari nchini.


"Sisi kama wadau wakubwa wa watetezi wa haki za binaadamu wakiwepo waandishi wa habari tutachangia mafunzo haya ili waandishi waweze kuripoti vyema uchaguzi mkuu kwa haki,bila upendeleo lakini wakibaki salama"alisema


Wakili ole Ngurumwa alisema THRDC kwa muda sasa imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa waandishi ikiwepo sheria za uchaguzi lakini pia mafunzo ya ulinzi na usalama kazini.


Awali Katibu Mkuu wa JOWUTA, Seleman Msuya alisema JOWUTA ndio chama pekee kinachotambulika kisheria nchini ambacho kinatetea maslahi ya wafanyakazi katika vyombo vya habari na masuala ya mazingira bora ya kazi zao.


Alisema hivyo THRDC kukubali kufanyakazi na JOWUTA hawajakosea na watakuwa pia wametimiza wajibu wao kuwasaidia watetezi wa haki za binaadamu kufanyakazi katika mazingira salama.


Hata hivyo alitoa wito kwa wadau wengine kusaidia wanahabari kupitia JOWUTA ambayo ina zaidi ya wanachama 400 nchi nzima.


Mwisho

Post a Comment

0 Comments