Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
HALMASHAURI ya jiji la Arusha imesaini MAKUBALIANO na wakandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi miwili yenye thamani ya sh,bilioni 9.4 ambayo ni ujenzi wa barabara ya lami ya ESSO hadi Longdong yenye urefu wa Kilometa 1.8 pamoja na ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa mikutano .
Mikataba hiyo imesainiwa mwishoni mwa wiki,katika eneo la Esso kata ya Ungalimited na kushuhudiwa na wakazi wa eneo hilo pamoja na mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda ambaye aliwataka wakandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza miradi hiyo kwa viwango na ubora unaotakiwa, ndani ya muda wa Makubalino huku akiwasisitiza wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kadri itavyohitajika.
" Mkandarasi ambaye hataendana na kasi ya mradi tutamtoa kwake anapokaa na kumhamishia kituo cha polisi awe anatokea hapo kuelekea katika eneo lake la kazi kutekeleza mradi". Alisema Makonda.
Mradi huo wa ujenzi wa barabara utatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3.2 pamoja na ukumbi wa kisasa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.2,kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.
Aidha alisema kuwa mkoa wa Arusha bado haujafanikiwa kwenye eneo la barabara hivyo kusainiwa kwa miradi hiyo kutasaidia kuunganisha kata mbili za Sokoni 1 na Unga limited kuwawezesha wananchi kupitia katika miundombinu kwa urahisi.
Awali kaimu Mhandisi wa jiji la Arusha,Sifa Edward akisoma taarifa ya miradi alisema kuwa mradi wa barabara ya Esso-Longdong unaotekelezwa na kampuni ya kichina ya JIANGXI GEO-ENGINEERING(GROUP) CORPORATION kwa thamani ya sh, bilioni 3.2 kwa muda wa Miezi sita.
Aidha alisema mradi mwingine wa ujenzi wa ukumbi wa mikutano unatekelezwa na kampuni ya wazawa ya STC CONSTRUCTION CO.LTD kwa kiasi cha sh,bilioni 6.09.
Alisema miradi hiyo ina malengo makubwa ikiwemo uendeshaji wa vikao vya ndani vya halmashauri kama chanzo cha mapato ya jiji kwa kukodisha kwa wadau mbalimbali .
Alisema jengo la mikutano likikamilika litakuwa na Kumbi nne ikiwemo utakaochukua watu 2000 kwa wakati mmoja huku akieleza lengo la mradi wa barabara ni kuchochea shughuli za kiuchumi baada ya wananchi kuweza kupita kirahisi tofauti na hapo awali.
Katika hatua nyingine Makonda ametoa wiki mbili kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arusha kuhakikisha nyaraka za ujenzi wa stendi ya kisasa zinakamilika na kusainiwa.
Ends..
0 Comments