CILAO Yamtaka Jaji Mkuu: "Linda kwa Wivu Mkuu Uhuru na Mamlaka ya Mahakama"
By Ngilisho Tv-ARUSHA
Shirika lisilo la kiserikali la Center for International Law Advocacy and Outreach (CILAO), limemuandikia barua Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, likimtaka kuchukua hatua za kulinda uhuru wa Mahakama dhidi ya kile walichokiita “kauli tata na ya kutishia haki” iliyotolewa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Katika barua hiyo yenye kichwa “Kukumbusha Kulinda kwa Wivu Mkuu Uhuru na Mamlaka ya Mhimili wa Mahakama,” iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa CILAO, Odero Charles Odero, shirika hilo limetaja kauli ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Muliro, kuwa kinyume na misingi ya utawala wa sheria.
Kauli ya Kamanda Muliro aliyotoa Aprili 17, 2025, ya kuonya watu wanaopanga kwenda Mahakama ya Kisutu kufuatilia kesi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Ndugu Tundu Lissu, ni tishio kwa haki ya kikatiba ya wananchi kushiriki na kufuatilia mwenendo wa kesi mahakamani,” amesema Odero katika barua hiyo.
Odero ameeleza kuwa hakuna sheria yoyote inayozuia wananchi kufika mahakamani kufuatilia kesi, hivyo kauli ya Jeshi la Polisi ni kinyume na Katiba na inaleta taswira ya kuingilia uhuru wa Mahakama.
“Hakuna sheria yoyote iliyotungwa na Bunge wala kanuni yoyote iliyotungwa na wewe, Jaji Mkuu, inayozuia mtu yeyote au kundi lolote kufika mahakamani kufuatilia mwenendo wa kesi ambayo ina maslahi naye,” Odero amesisitiza.
Kwa mujibu wa barua hiyo, CILAO imeomba Jaji Mkuu atoe maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha linazingatia sheria za nchi na kuheshimu uhuru wa Mahakama kama mhimili huru wa dola.
“Tunakuomba, Mheshimiwa Jaji Mkuu, uwe na wivu mkuu wa kulinda Mahakama na kamwe usiruhusu mhimili huu kuwa Jehanamu kwa wananchi, bali uendelee kuwa faraja na kimbilio la watu,” amesema Odero.
Barua hiyo pia imetumwa kwa nakala kwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mathew Pauwa Mhina Mwaimu.
CILAO ni shirika linalojihusisha na utetezi wa haki za binadamu, utawala wa sheria, na ushirikishwaji wa wananchi katika mifumo ya haki nchini Tanzania.
Ends...
0 Comments