By Ngilisho Tv-SHINYANGA
BABU anayefahamika kwa jina la Maganga Mungo mkazi wa Kijiji cha Shatimba wilayani Shinyanga, anadaiwa kumua mjukuu wake wa siku mbili kwa kumpigiza chini, kwa kile kilichodaiwa kuwa binti yake amezaa na baba yake mdogo, kitendo ambacho hakukubaliana nacho.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Shatimba, Kalonga Shilu, amesema tukio hilo limetokea Aprili 11, mwaka huu majira ya saa tatu usiku.
Amesema babu huyo aliomba apewe mjukuu wake ili amuone, baada ya kupewa akasema anamua sababu ni aibu katika familia binti kuzaa na baba yake mdogo,ndipo akampigiza chini na kufariki dunia.
“Familia hii ilikuwa na mgogoro wa muda mrefu kutokana na binti kuolewa na baba yake mdogo, na alipozaliwa mtoto, ndipo baba yake mzazi akashikwa na hasira na kuamua kwenda kumua mjukuu wake, ambaye alikuwa ameshafikisha siku mbili tangu azaliwe,”amesema Shilu.
Amesema baada ya kutokea tukio hilo, babu yake alikimbia kusikojulikana, na walitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua zaidi za kisheria zipate kuchukuliwa.
Mkazi wa Kijiji cha Shatimba, Paul Maige, amesema amesikitishwa na tukio hilo la mauaji ya kinyama, kwa kuuliwa mtoto ambaye hana hatia na kuomba hatua za kisheria zichukuliwe ili kusije endelea kutokea matukio kama hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alipotafutwa kuhusu suala hilo amesema bado hajapokea taarifa zake.
Aidha, ameahidi kulifuatilia kisha kulitolea taarifa kamili kwa umma haraka iwezekanavyo.
Chanzo ,Malunde
0 Comments