WANANCHI 600 ARUMERU KUIBURUZA TANROADS MAHAKAMANI,WAKILI WA SAMIA LEGAL AID ASIMAMA NAO

Na Joseph Ngilisho ARUSHA 


WANANCHI zaidi ya 600 kutoka kata 5 katika halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha ,wanakusudia kuipeleka mahakamani wakala wa barabara Tanzania Tanroads Mkoani hapa,wakilalamikia kutolipwa fidia baada ya kubomolewa nyumba zao kupisha mradi wa barabara ya Mianzini-Timbolo . 


Wakizungumza kwa jazba katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Ilikiding'a wilayani humo, mbele ya wakili wa chama cha Mawakili Tanganyika (TLS),Baraka Sulus kutoka Kampeni ya mawakili wa msaada wa kisheria wa Mama Samia Legal Aid.


Wananchi hao kutoka kata za Oltroto ,Ilboru,Sambasha ,Kiranyi na Ilikiding'a walimwomba wakili huyo kuwasaidia kufikisha kiliochao kwa Rais Samia Suluhu na kupata haki yao Tanroads kwani baada ya kupitiwa na mradi huo na Nyumba zao kubomolewa baadhi yao wameshindwa kutengeneza makazi mengine ya kuishi na kufanya maisha yao kuwa magumu.

Baadhi ya wananchi hao, Richard Josiya,Isaya Mollel na Godson Mwikano walidai kuwa kabla ya kuanza mradi huo wa barabara kuna timu kutoka makao makuu ya Tanroads walifika katika maeneo yao na kuwapatia semina ya namna barabara itakavyokuwa ikiwa ni pamoja na kuhakiki maeneo ya mradi na kuwahakikishia fidia.


"Baada ya hapo zilikuja tena timu zingine kwa ajili ya kufanya tathimini na kuandikisha majina ya waathirika wa mradi na wale  walioridhika na kiwango cha malipo walisainishwa na kutakiwa kusubiri malipo,lakini hadi sasa ni muda mrefu na hakuna kinachoendelea na mbaya zaidi tumesikia malipo yetu hayatakuwepo tena "


Aidha walimtupia lawama mbunge wao Lembris Noar kwa kushindwa kuwatetea kupata haki yao badala yake amekuwa akiwakajeri na kuwakatisha tamaa kwamba hawatalipwa chochote Kwa sababu walikuwa wamejenga ndani ya barabara ya akiba jambo ambalo wameapa kutomchagua tena katika kipindi cha uchaguzi kama mbunge wao.

 

Mmoja ya wananchi hao William Loishiye Kimti  ambaye ameathirika kwa kubomolewa maduka yake na nyumba alidai kuwa zoezi hilo la upanuzi wa barabara lilifanyika mwaka 2019 na wananchi hao akiwemo yeye walifanyiwa tathimini ya fidia na kuandikishwa kulipwa.


"Mimi nilifanyiwa tathimini na kusaini malipo ya fidia zaidi ya kiasi cha shilingi milioni 30 lakini hadi leo sijalipwa na baadaye tulipata taarifa kwamba Tanroads haitatulipa, jambo ambalo limetusikitisha sana"Alisema.


Mwananchi Mwengine kutoka kata ya Sambasha Isaya Mollel alisema kabla ya zoezi la upanuzi wa barabara kuna timu ilikuja kutoka Tanroads makao makuu na kufanya mkutano na wananchi wakiwaeleza wananchi namna zoezi la upanuzi litakavyo kuwa.


"Timu hiyo walikuja na kutupatia elimu katika MIKUTANO mbalimbali na kutueleza kuwa wamekuja kutufundisha kwamba watachukua mita tano wakiwa na maana kwamba kila upande watachukua mita mbili na nusu"


"Baada ya timu hiyo kumaliza iliondoka na  kuja timu nyingine ya Tathimini na kila mwananchi aliambiwa asimame katika eneo lake na kupigwa picha na kuandikishwa ikiwemo kupewa namba, baada ya zoezi hilo kumalizika ilikuja timu nyingine ya uhakiki"


Alisema hadi sasa wamebaki na fomu zao za malipo lakini Tanroads wamekataa kuwalipa kwa madai kwamba hawastahili .


Hata hivyo alisema wakati timu ya Mawakili kutoka Kampeni ya msaada wa kisheria wa Mama Samia Legal Aid waliokuja jijini Arusha katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani,walifanikiwa kuonana na rais wa TLS Bonface Mwambukusi ambaye aliwasikiliza akiwemo meneja na Tanroads mkoa wa Arusha na kuwambia kwamba wanastahili kulipwa fidia.

Kwa upande wake wakili Sulus alisema nia ya mama Samia Legal Aid,ni kusaidia wananchi walioonewa  ama kutojua sheria na kwamba wao kama wanasheria amebaini kwamba wananchi hao wakidanganywa na kubomoa maeneo yao wenyewe kupisha mradi kwa madai ya kulipwa fidia jambo ambalo hadi sasa halijafanyika.


Alisema sheria kwenye mambo ya utoaji ardhi ipo wazi kwamba katika mradi wowote unaotaka kuufanya katika ardhi ya huyo uliyemkuta unatakiwa kumlipa kabla ya kuanza kutekeleza mradi wako na malipo hayo lazima yalipwe kwa wakati,yawe halali na stahiki kwa thamani ya ardhi ya wakati huo.


Alisema amejipanga kwenda Tanroads kuwakilisha malalamiko ya wananchi ili kujua nini kimekwamisha malipo ya wananchi hao.


Meneja wa Tanroads Mkoa wa Arusha Mhandisi Reginald Masawe alipohojiwa alisema kwamba wananchi hao hawastahili malipo ya fidia kwa kuwa walijenga ndani ya eneo la barabara ya mradi.


Hata hivyo alishindwa kufafanua namna wananchi walivyofanyiwa tathimini na kukabidhiwa fomu za malipo na baadaye kuambiwa hawatalipwa na kwamba waliofanya tathimini walikuwa ni wahuni.








Ends....















Post a Comment

0 Comments