TCRA YABAINISHA MAENEO YENYE MAWASILIANO HAFIFU NCHINI!

By Ngilisho Tv 


Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeainisha maeneo yenye huduma hafifu na yasiyo na huduma za mawasiliano ya simu, utangazaji na intaneti.


Hatua hiyo ni baada ya kufanya utafiti nchini kote na imewasilisha taarifa ya utafiti huo kwa huduma ili waboreshe huduma kwenye maeneo hayo, imefahamika.


Taarifa ya TCRA kuhusu hali ya mawasiliano Tanzania ndani ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeyaainisha maeneo hayo ni pamoja na yasiyofikiwa na mawimbi ya utangazaji.


Taarifa hiyo, iliyotolewa Machi 24, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, ambaye alisema asilimia 79 ya watu wanafikiwa na huduma za utangazaji wa redio wa FM na kwamba mawimbi hayo yanafika asimilia 56 ya eneo la kijiografia.



“Mawimbi ya televisheni mfumo wa ardhini (DTT) yanafikia asilimia 58 ya watu na asilimia 33 ya eneo la nchi. Mfumo wa Televisheni kwa Satelaiti (DTH) umeenea kwa asilimia 100 miongoni mwa watu na kijiografia,” amesema.


Aidha, TCRA imetoa leseni limbikizi za utangazaji 659 kati ya mwaka 2003 na Desemba 2024 na kwamba kati ya hizo huduma za utangazaji televisheni zilizolipiwa ni 38, televisheni zinazolipiwa 29 na televisheni za waya 58.


“Leseni za redio ngazi ya taifa, mkoa na wilaya zimefika 233, na redio za jamii 17. Nyingine ni za maudhui ya televisheni mitandaoni 199 na redio mitandaoni 10,” amesema.


Aidha, leseni sita zilitolewa kwa watoa huduma za kutengeneza na kuandaa maudhui, na 66 kwa blogu za maudhui ya habari.


“Pamoja na kuenea huduma za utangazaji, Tanzania imejipanga kutekeleza mambo mapya matatu kuhakikisha matangazo yanafikia wasikilizaji na watazamaji wengi zaidi, na pia kuboresha ubora huduma za maudhui,” amesema.



Aidha, kwa kipindi hicho Tanzania ilipata nafasi anga za juu Nyuzi 16, kwa ajili ya mzunguko wa satelaiti yake ya kwanza ya mawasiliano.


Mafanikio haya yalipatikana kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano ya Redio, uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu mwaka 2023.


“Vilevile miundombinu ya utangazaji inawekwa maeneo yenye ugumu kufika mawimbi ya redio na televisheni, na ambayo kwa wawekezaji hayana ‘mvuto’ kibiashara na hivyo kutokufikiwa na huduma ipasavyo,” amesema.


Aidha, amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), unatekeleza miradi hiyo na kwamba TCRA na wadau wa maudhui wanajitahidi kuimarisha mfumo wa upatikanaji wa maudhui stahiki kupitia mitandao yanayokidhi mahitaji ya wananchi kiutamaduni, kijamii na kuwezesha kujiendeleza kiuchumi.


“TCRA inasimamia utangazaji Tanzania Bara. Ina kamati mahsusi inayoshughulikia maudhui kwa kufuatilia uzingatiaji maadili na kanuni za maudhui ya redio, televisheni na mtandaoni kwa wenye leseni ya mamlaka.



Aidha, TCRA inashirikiana na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, kwenye kuendeleza maadili na weledi kwenye uaandaji na utoaji maudhui, bodi hiyo, iliyozinduliwa Machi 3, mwaka huu, inatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha sekta ya utangazaji inazingatia maadili, kanuni na weledi katika utendaji kazi wake.

Post a Comment

0 Comments