Na Joseph Ngilisho -ARUSHA .
NAIBU Waziri wa Afya ,Dkt Godwin Mollel amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kifua Kikuu kutoka wagonjwa 306 kwa kila watu 100,000 mnamo 2015, hadi wagonjwa 183 kwa kila watu 100,000 kwa mwaka 2023, ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 40.
Ameyasema hayo mapema leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha katika maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani 2025 ambayo kitaifa yamefanyika jijini Arusha.
Dkt Mollel alisema kuwa ,vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu vimepungua kutoka vifo 56,000 mwaka 2015 hadi vifo 18,400 mwaka 2023, hii ikiwa ni sawa na punguzo la asilimia 68.
“Kiwango hiki kimepelekea nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi 13 duniani zilizo katika hatua sahihi kufikia lengo la dunia la kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 50 na vifo kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2025 na hivyo kuwa katika njia sahihi ya kutokomeza Kifua Kifuu ifikapo 2030.”alisema .
Hatua hizi zimechangiwa na jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha huduma za Kifua Kikuu nchini, ikiwemo kuongeza wigo wa mtandao wa huduma za uchunguzi na upimaji Kifua Kikuu, ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya Kifua Kikuu na pia upatikanaji madhubuti wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya huduma za Kifua Kikuu nchini.
Alifafanua kuwa, Tanzania inaungana na Ulimwengu mzima katika kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani ambapo siku hii imetengwa kwa ajili ya kuongeza jitihada na mikakati ya kutokomeza ugonjwa huu ifikapo Mwaka 2030.
“Siku hii hutumika kuchagiza hamasa na elimu kwa jamii ili kuufahamu zaidi ugonjwa wa Kifua Kikuu, hususan njia za kujikinga na pia kuendelea kuikumbusha jamii kuhusu wajibu wao katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.”
Kwa mwaka huu Kauli Mbiu ya siku ya Kifua Kikuu Duniani, inasema, “Kwa Pamoja Tunaweza Kutokomeza Kifua Kikuu: Azimia, Wekeza, Timiza”. Kauli Mbiu hii imejikita katika kuhamasisha jamii na wadau wote juu ya wajibu wao katika kuchochea jitihada za kutokomeza ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini.
Awali Meneja mpango wa Taifa wa kifua kikuu na Ukoma Dkt Riziki Kisonga alisema kuwa,Takwimu hizo zinatupa matumaini ya kufikia lengo la kutokomeza Kifua Kikuu Tanzania ifikapo 2030,ambapo lengo hili linaweza lisifikiwe kama hatutawekeza katika kutatua changamoto zinazorudisha nyuma jitihada zetu.
Ametaja Changamoto hizi ni uwepo wa Uelewa mdogo wa jamii kuhusu dalili za ugonjwa wa Kifua Kikuu unaopelekea watu kuchelewa kuchukua hatua mapema na hivyo kuendeleza mnyororo wa maambukizi katika jamii yetu.
Aidha ametaja changamoto nyingine kuwa ni Kushindwa kuyafikia makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu kama vile wachimbaji wadogo wadogo, wavuvi, wafungwa na mahabusu, waishio katika makazi holela na wengine.
Ametaja changamoto nyingine kuwa ni Ushiriki finyu wa sekta binafsi katika kusaidia jitihada za kutokomeza Kifua Kikuu nchini, mathalan kati ya takribani vituo binafsi 3,000 vya kutolea huduma za afya viliyopo nchini, ni asilimia 16% tu ndio vinashiriki katika kutoa huduma za Kifua Kikuu.
“Katika kukabiliana na changamoto hizi na nyingine, Wizara, kwa kushirikiana na wadau, kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Desemba 2024 hadi Machi 2025, inaendesha kampeni maalum katika Halmashauri 76 zilizopo katika mikoa 9 nchini, Kampeni hii inalenga kuchochea kasi ya kuibua wagonjwa na kuwaweka katika matibabu, hususan makundi yaliyo katika hatari ya kuugua Kifua Kikuu na pia kuongeza ufahamu juu ya ugonjwa huu katika jamii, Hadi sasa matokeo ya awali yanaonesha kuwepo kwa mafanikio katika kampeni hii.”amesema .
Dkt Kisonga ameongeza kuwa,kupitia kampeni hii, mpaka sasa, jumla ya wagonjwa 9,585 wa Kifua Kikuu wameibuliwa na kuwekwa kwenye matibabu, ikiwa ni sawa na asilimia 66% ya lengo la kampeni la kuibua wagonjwa 14,471.
Aidha, wagonjwa wa Kifua Kikuu Sugu 36 wamebainika na kuwekwa katika matibabu,kuongeza hamasa na utashi juu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri, kampeni hii ilizinduliwa Kitaifa lakini pia kila mkoa nao uliweza kufanya mkutano mkubwa wa wadau ulioratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa husika.
“Kampeni hii imetupa somo kubwa katika kutumia mbinu mbalimbali za kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Kifua Kikuu nchini, ni matumaini yangu mikoa mingine iliyobaki itaiga mfano huu na kutekeleza katika mikoa yao. Aidha mikoa tisa (9) iliyoshiriki iendeleze jitihada hizi pasipo kurudi nyuma.”amesema Dokta Kisonga .
“Hivi karibuni tulipokea waraka kutoka Serikali ya Marekani unaelekeza kusitishwa kwa baadhi ya afua za afya zilizokuwa zinafadhiliwa na serikali hiyo. Hatua hii imepelekea kuleta sintofahamu katika jamii yetu, hususan katika magonjwa haya ya UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu.
"Nipende kuwahakikishia kuwa, Serikali yenu sikivu ya Awamu ya Sita (6) chini ya Mhe Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kukabiliana na hali hii, Kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Serikali imefanya tathimini ya kina ili kubaini pengo litakalojitokeza na kutengeneza mpango mkakati wa kutatua changamoto hizi,kwa upande wa Kifua Kikuu, nimetaarifiwa kuwepo kwa mkakati wa Kujumuisha shughuli za utokomezaji wa Kifua Kikuu na afua zingine za afya katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kwa kutumia rasilimali zilizopo.”alisema .
Alifafanua kuwa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa,vitendanishi na vifaa tiba kwa ajili ya huduma za Kifua Kikuu na magonjwa mengine, matibabu dhidi ya magonjwa haya yataendelea kutolewa bila malipo kwa wakati wote,kuongeza hamasa na elimu ya Kifua Kikuu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni zenye lengo la kuongeza uibuaji wa wagonjwa na kuwaweka kwenye matibabu.
Kushirikisha sekta zote za umma na binafsi katika kuongeza rasilimali za kupambana na Kifua Kikuu nchini. Msisitizo utawekwa katika utekelezaji wa mkakati wa uwajibikaji wa Kisekta wa mapambano dhidi ya Kifua Kikuu unaosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ujulikanao kama Mult-Sectorial Accountability Framework for TB (MAF-TB).
“Tunapoadhimisha siku ya leo, nichukue fursa hii kusisitiza kuwa, kwa sasa Wizara inajikita katika kutekeleza afua jumuishi za kupambana na magonjwa mbalimbali, hivyo kusitisha mtindo wa kupambana na ugonjwa mmoja mmoja,hii italeta tija na kuongeza ufanisi kwa rasilimali chache tulizonazo Kupitia jukwaa hili.”
Aidha ametoa rai kwa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa zijipange kutengeneza mkakati jumuishi wa utekelezaji wa afua ili kutumia kwa ufanisi na tija rasilimali chache zilizopo.
Aidha ameitaka Mikoa na Halmashauri zihakikishe Watumishi wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) walioajiriwa watumike kwa kuzingatia muongozo na watengewe muda na rasilimali katika kushughulikia utekelezaji wa afua za magonjwa yote ikiwemo Kifua Kikuu.
Ends..
0 Comments