SAMIA LEGAL AIDS YATATUA MIGOGORO 136 KATI YA 677 MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI ARUSHA

 Na Joseph Ngilisho-Arusha


JUMLA ya Migogoro  677 ilimepokelewa  kupitia  kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Samia Legal Aid),ambapo kati ya hiyo migogoro 136 imetatuliwa huku idadi kubwa ikihusisha madai ya Mali.

Kampeni hiyo imeweka rekodi baada ya kufanikiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 1800 katika mikoa 22 nchini ambayo imeshatembelewa.

Akizungumza leo Machi 7, 2025 Mkurugenzi wa kampeni ya Samia Legal Aid, Ester msambazi amesema katika maonyesho yanayoendelea jijini Arusha kuelekea siku ya mwanamke duniani, wameshapokea migogoro 677 hadi jana machi 7,2025 na wataendelea hadi machi 11 Mwaka huu.


Alisema miongoni mwa migogoro hiyo, migogoro 136 imefanikiwa kutatuliwa kwa wenye migogoro kusameheana na kupeana mikono huku baadhi ya migogoro iliyoko ngazi ya mahakama wahusika wameandikiwa hati za mahakama na kutakiwa kufika mahakamani.

“Katika maonyesho haya tumefanikiwa kupokea migogoro 677 na kupatia ufumbuzi migogoro 136, ambapo waliofika tumewaandikia makubaliano na kuwashauri kufika mahakamani wale wanaopaswa kufika huko,”


Alisema tofauti na migogoro ambayo wamekuwa wakiipokea kutoka katika mikoa mingine nchini, migogoro mingi ya Arusha inatokana na watu kudaiana mali, huku mikoa mingine migogoro ya mirathi imeonekana kuwa kinara namba mbili baada ya migogoro ya ardhi.
 
“Arusha kumekuwepo na changamoto kubwa ya migogoro ya madai baada ya migogoro ya ardhi na wanaofikisha madai wengi ni wanaume, tofauti na mikoa mingine tuliyotembelea, hata hivyo tumefanikiwa kutatua migogoro mingi na tunaendelea kuitatua,”amesema.
 
Msambazi amesema migogoro iliyobaki inaendelea kufanyiwa kazi na jopo la wanasheria walioko katika kampeni hiyo na endapo wahusika hawajaridhika na majibu wanayopatiwa huruhusiwa kwenda katika taasisi zingine kutafuta haki zaidi.
 
“Sisi tumekuja hapa kutoa haki, hakuna hata mmoja ambaye tunafanya upendeleo lakini kuna baadhi ambao wao huwa hawataki kushindwa wala kupatanishwa wakiona hawawezi kupatana sisi tunawaruhusu kwenda mbele kutafuta haki zaidi,”amesema.
 
Alisema kampeni hiyo itaendelea kwa siku tatu hadi Machi 11,2025  baada ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yatakayofungwa na Rais  Samia Suluhu Hassan .
 

Ends...

Post a Comment

0 Comments