PSSSF na AICC Kujenga Ukumbi wa Mikutano wa KMICC
Na Joseph Ngilisho -ARUSHA
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) zimetiliana saini ya utekelezaji wa mpango mahususi wa ujenzi wa ukumbi mkubwa wa kisasa wa Mikutano wa Mt Kilimanjaro(KMICC)jijini Arusha, yakiwa ni maono ya Baba wa Taifa Hayati Julius Nyerere na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameshuhudiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo ,wakati wa hafla ya uwekaji saini wa Ukumbi huo utakao kuwa na uwezo wa kuchukua watu 5000 kwa mkupuo mmoja.
"Rais Samia ameona kwa uono mpana kabisa kuna fursa nyingi katika utalii wa vikao, incentives, mikutano na maonesho (meetings, incentives, conferences and exhibition-MICE) ambazo hazijatumiwa vizuri kutokana na miundombinu duni"
"Hivyo, ujenzi wa ukumbi huu ambapo ameelekeza pia ijengwe na hoteli isiyopungua vyumba 500 pembezoni mwa ukumbi ni mwendelezo wa Serikali yake wa kutatua changamoto katika sekta ya utalii", Balozi Kombo alisema.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana, ajira na wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) ametoa wito kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii PSSF na AICC kuhakikisha wanasimamia vyema mradi wa ujenzi wa ukumbi huo utakao kuwa na uwezo wa kubeba watu 5,000 kwa mara moja.
Alisema mchakato wa ujenzi wa kituo hicho ni matokeo ya miongozo mbalimbali inayoongozwa na dira ya taifa ya maendeleo ya mwaka 2025.
"Utekelezaji huu ni maelekezo ya ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020 hadi 2025 inayotuelekeza kujenga ukumbi mkubwa wa mikutano utakaoweza kuileta Dunia Tanzania", Alisema.
Aidha, alisema anafarijika kuona taasisi ya PSSF ilivyoingia makubaliano mazuri na kituo cha Mikutano cha AICC katika utekelezaji wa mradi huu ambao unatakiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.
"Nitahakikisha mradi huu unakamilika kama ambavyo tumekubaliana kwenye mkataba ili uweze kuleta tija kwa Watanzania"
Aliongeza kuwa Mradi huo ni wa kujivunia kwani unakwenda kuweka alama kubwa Tanzania na unajengwa na watanzania wenyewe na utasaidia kuchochea fursa za kiuchumi katika mji wa Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, pamoja na kumpongeza Mhe. Rais kwa kutoa ruksa ya ujenzi wa kituo hicho, aliikumbusha hadhira kuwa ujenzi wake ni maelekezo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 inayoelekeza umuhimu wa kujenga mazingira wezeshi na muhimu kwa ustawi wa Taifa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni pamoja na Maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala (CCM) ya mwaka 2021.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Msajiri wa Hazina, Bi. Neema Musomba alisema, “Msajili wa Hazina anapongeza ushirikiano wa PSSSF na AICC, na kuwa ofisi ya Msajili wa Hazina wakati wowote itakuwa tayari kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.”
Watendaji wakuu wa PSSSF na AICC kwa nyakati tofauti walisisitiza kutimiza wajibu wao ili kuhakikisha mradi huokimkakati unakamilika kama ilivyopangwa.
Ends...
0 Comments