Rais Samia aboresha huduma ya Maji Matumbulu
Na. Emanuel Charles, MATUMBULU
DIWANI wa Kata ya Matumbulu, Emmanuel Chibago ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya sekta ya afya, elimu, ujenzi wa ofisi ya kata pamoja na mradi wa maji ambao mpaka sasa serikali imefanikiwa kujenga visima 12 vinavyotoa huduma ya maji kwa wananchi wa kata hiyo.
Akiongelea mafanikio ya serikali katika kipindi cha miaka minne kwa waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2021 hadi sasa katika Kata ya Matumbulu, Diwani Chibago alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kupeleka miradi ya maendeleo katani hapo. Alisema kuwa serikali imechimba visima 12 vya maji ukilinganisha na awali kilikuwepo kisima kimoja tu kikihudumia kata nzima. “Nipende kuipongeza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu mpaka sasa katika Kata ya Matumbulu wananchi hawahangaiki na maji tena tofauti na hapo mwanzo palikuwa na kisima kimoja cha maji ambacho kilikuwa ni tegemeo kwa wananchi wote wa Kata ya Matumbulu” alisema Chibago.
Nae Coletha Kapinga, Mtaalamu kutoka RUWASA na Mhasibu wa mradi wa maji Kata ya Matumbulu alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka mradi mkubwa wa maji ambao unahudumia mitaa mitatu ya Kawawa, Nyerere na Mwongozo. “Mradi huu ni mkubwa, licha ya ukubwa wake unahudumia idadi ya watu 4,120 ambao wananufaika na maji haya. Hizi zote ni jitihada za Rais wetu kutuletea mradi huu uliogharimu shilingi 360,000,000. Tunamshukuru sana, baada ya kupata mradi huu wananchi wanapata maji safi na salama” alisema Kapinga
Kwa upande mwingine Amosi Chipanyanga, ambae ni mkazi wa Mtaa wa Mpunguzi ‘A’, Kata ya Matumbulu alimshukuru Rais kwa kuwapelekea mradi wa maji ambapo wakati wa nyuma walikuwa wanahangaika kwa uhaba wa maji. “Tunashukuru kuletewa mradi huu na Rais, Samia Suluhu Hassan kwasababu tulikuwa tunapata shida sana wakati wa nyuma, lakini kwasasa tumepata manufaa makubwa sana kutokana na mradi huu watu wanapata huduma kwa wakati muafaka” alimalizia Chipanyanga.
MWISHO
0 Comments