MZEE WA MIAKA 60 DNA YAMUUMBUA AHUKUMIWA JELA MIAKA 30,ALIMBAKA MWANAFUNZI NA KUMZALISHA,SHIRIKA LA MEMUTE LAINGILIA KATI LAMREJESHA SHULE AKIWA MAMA, MTUHUMIWA ALIJARIBU KUPELEKA SODA , SUKARI NA KOMDOO!

 Na Joseph Ngilisho- ARUSHA 


MAHAKAMA ya  Sekei wilaya ya Arumeru Mkoa wa Arusha,imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela,mzee wa miaka 60, Asorael Kalaine Mkazi wa Maruango wilayani humo,mara baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Maruango iliyopo wilayani Arumeru.

Kesi hiyo ya kubaka namba 33 ya mwaka 2023,iliwezeshwa na shirika la MEMUTE organization linalojihusisha na utetezi wa haki za watoto na wanawake baada ya kubainika kwamba suala hilo linataka kumalizwa  kienyeji baada ya mtuhumiwa kufanikiwa kupeleka dume la Kondoo kuomba msamaha.

Uamuzi wa kesi hiyo ulitolewa jana Machi 28,2025 baada ya mahakama hiyo kujiridhisha pasipo shaka na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ikiwemo kipimo cha vina saba (DNA),kilichotambua mahusiano kati ya mtuhumiwa na mtoto baada ya kuzaliwa.

Akiongea nje ya Mahakama, Mkurugenzi wa shirika la MEMUTE, Rose Njilo aliishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki katika uamuzi wa shauri hilo ambalo hata hivyo alidai limechukua muda mrefu kumalizika ,akidai hukumu hiyo itakuwa fundisho kwa wanaume wengine wanaoendekeza vitendo vya ukatili dhidi  ya watoto wa kike.

"Tunaishukuru mahakama tumepata mafanikio katika safari ndefu ya kesi ya ubakaji iliyomhusu mzee Asorael Kalaine mwenye miaka 60 ambaye alimbaka binti wa miaka 16 mwanafunzi wa kidato cha kwanza baada ya kumrubuni na kumvutia ndani ya mgahawa wake na kumbaka na kisha kumpatia ujauzito"


Alisema kwamba haikuwa rahisi   suala hilo kufika kwenye vyombo vya kisheria na kumalizika ukizingatia jitihada zilizokuwa zikiendelea kwa upande wa mtuhumiwa kutaka jambo hilo limalizike nyumbani baada ya kufanikiwa kuwarubuni kwa kuwapatia dume la Kondoo .


"Katika ufuatiliaji wa Kesi hiyo tulikumbana na Changamoto nyingi ikiwemo ya ucheleweshaji wa uendeshaji wa shauri hilo ambalo upande wa mahakama mara kwa mara ilikuwa ikiahirisha kesinhiyo bila sababu za msingi na wakati huo sisi kama taasisi tulichukuwa jukumu na kumlea mwathirika katika kituo chetu cha MEMUTE Girls ili kulinda ushahidi hadi mtoto alipojifungua"

Rose kupitia shirika lake la MEMUTE organization  wamefanikiwa kumrejesha masomoni binti huyo baada ya kujifungua salama ambapo kwa sasa akiwa chini ya uangalizi wa shirika hilo,anasoma kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Maruango iliyopo wilayani humo na mtoto wake  anaendelea vizuri akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu akiwa chini ya uangalizi wa bibi yake.

Akizungumzia namna alivyopokea hukumu hiyo mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) aliishukuru mahakama hiyo kwa kutenda haki akidai ni mfano kwa wababa wenye tabia ya kurubuni kingono watoto wadogo wa kike bila kujali ndoto zao za kusoma.

Akisimulia namna alivyokumbwa na mkasa huo wa kubakwa na mzee huyo Asorael Kalaine (60)mwaka 2023,alisema kuwa alibakwa baada ya mzee huyo kumwita ndani na kuanza kumwingilia na kisha kumtisha kwamba iwapo atamwambia mtu yoyote ataweza kumuua yeye na familia yake jambo lililomfanya aingiwe hofu na kukaa kimya.

"Nilikuwa nimepeleka maziwa mzee aliniita na kuniomba niingie ndani na nichukue chombo cha kuhifadhia maziwa akisema atayanunua yote, nilipoingia  alinifuata na kunivutia ndani na kuanza kunibaka"

Alisema aliendelea na masomo yake kama kawaida ila baadaye alijigundua ana mimba na kumtaarifu mhusika ambaye alimshauri waitoe kwa kumpatia dawa za kienyeji ,alitumia dawa hizo lakini mimba haikutoka hadi alipogunduliwa na walimu wake akiwa na ujauzito wa miezi nane .

"Alipogundua nina ujauzito,alianza kunipatia dawa za kienyeji kwa lengo la kutoa ujauzito,lakini hazikufanikiwa na mimba iliendelea kukua"

Mama mzazi wa binti huyo , Neema Joseph mkazi wa Maruango ,alidai kwamba wakati shauri hilo likiwa linaendelea mahakamani upande wa mtuhumiwa walipambana kutaka jambo hilo limalizike nyumbani ikiwa ni pamoja na jaribio la kupeleka kreti mbili za soda, Sukari na dume la Kondoo , wakiwa na nia ya kuomba msamaha ili wayamalize kimyakimya

"Mimi niliwakatalia nikawaambia haiwezekani hakimu aendeshe kesi mahakamani na mimi niendeshe kesi nyumbani"

Alisema shauri hilo liliendelea mahakamani baada ya jaribio la mtuhumiwa kugonga mwamba hadi hukumu ilipotolewa .

Kabla ya  hukumu , mtuhumiwa alipewa nafasi ya kujitetea ambapo aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa yeye ni mzee ana umri wa miaka 60 na akitoka atakuwa na miaka 90 hivyo anaweka kufia gerezani.

Hata hivyo mahakamani hiyo haikuzingatia madai hayo na kuamua kumhukumu bila huruma kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 adhabu ambayo tayari ameanza kuitumikia.

Enda...

















Post a Comment

0 Comments