Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mhandisi Anthony Sanga, amewashauri wananchi wa Kanda ya Kaskazini kupendana na kuthamini mshikamano wa kifamilia ili kupunguza changamoto ya migogoro ya ardhi inayoendelea katika eneo hilo.
Akizungumza leo jijini Arusha katika banda la wizara hiyo kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Sanga amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi katika mkoa wa Arusha na mikoa jirani inatokana na migawanyo ya urithi, ugomvi wa kifamilia, na tabia ya kubagua watoto wa kike katika masuala ya urithi wa ardhi.
"Chanzo kikubwa cha migogoro ya ardhi ni migogoro ya kifamilia—watoto kugombana na watoto wenzao, wazazi kugombana na watoto wao, na mara nyingi ubaguzi wa watoto wa kike katika mirathi. Tunawasihi wananchi kuwa na upendo na mshikamano wa kifamilia, kugawa haki sawa za urithi bila ubaguzi wa kijinsia, na kuacha tabia ya kugombana isiyo na tija," amesema Sanga.
Aidha, amekemea vikali tabia ya kubagua watu kwa misingi ya ukabila katika umiliki wa ardhi, akisisitiza kuwa ardhi yote nchini ni ya Watanzania wote na hakuna kabila lolote linalostahili kumiliki ardhi kwa upendeleo.
"Tanzania haina ardhi ya kabila fulani. Sera na sheria zetu zinatambua kuwa ardhi ni kwa Watanzania wote, hivyo kila mtu ana haki ya kumiliki na kuishi popote bila kujali anatoka kabila gani," amesisitiza Sanga.
Pia amewataka wananchi wanaoshindwa kesi zao za ardhi mahakamani kuridhika na maamuzi ya kimahakama badala ya kuendelea kuhangaika au kutafuta njia za mkato.
"Hatuwezi kuingilia maamuzi ya mahakama, lakini tunawasikiliza na kuwashauri wananchi. Pale tunapobaini mtu hana haki katika mgogoro wa ardhi, tunamweleza ukweli na kumuomba aridhike na maamuzi yaliyotolewa," amehitimisha.
0 Comments