By Ngilisho Tv
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora linamshikilia askari wa usalama barabarani, WP 8032 PC Victoria, kutoka Wilaya ya Igunga, kwa kushiriki katika uchotaji wa mafuta kutoka kwa lori lililopata ajali.
Tukio hili linazua maswali mengi kuhusu maadili ya kazi ya polisi na usalama wa jamii, huku likikumbusha ajali kubwa ya mafuta iliyotokea miaka sita iliyopita mjini Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao, alieleza kuwa askari huyo alifika katika eneo la ajali, lakini badala ya kudhibiti wananchi waliokuwa wakichota mafuta kutoka kwa lori lililoharibika, alionekana akitoa dumu kwa mmoja wao ili aendelee kuhifadhi mafuta hayo.
Kamanda Abwao alisema, "Askari huyu hajazingatia taratibu na maadili ya kazi yetu kwa sababu badala ya kuonya wananchi, yeye anashiriki."
Ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Igogo, barabara ya Igunga-Nzega, ambapo lori la mafuta liligonga kwa nyuma lori la mahindi, kisha kupoteza mwelekeo na kugonga lori jingine. Polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hili.
0 Comments