Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WANAWAKE na vijana wanaojishughulisha na uuzaji wa bidhaa maeneo ya mipakani wametakiwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ili waweze kushiriki kikamilifu katika soko huru la Afrika linalolenga kuwakwamua kiuchumi.
Aidha katika kukabiliana na vikwazo visivyo vya kiforodha wanavyokumbana navyo, sekta ya umma na sekta binafsi imekutana na vijana na wanawake wanaofanya biashara za mazao ya vyakula mipakani na namna ya kushughulikia vikwazo visivyo vya kiforodha .
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Ijumaa Machi 28, 2025 na Afisa biashara mkoa wa Arusha, Njivaine Mollel wakati akifungua mafunzo ya majadiliano uliohusisha vijana zaidi ya 100 kutoka mikoa ya Arusha na Manyara, wanaofanya biashara mipakani.
Aliwataka Wafanyabiashara hao kushiriki mafunzo ya namna hiyo yanayotolrwa na AGRA ili kuwajengea uelewa wa kufanya biashara mipakani na kutumia fursa hiyo ukizingatia kwamba nchi wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki zimeondoa vizuizi.
Naye Mkurugenzi wa TCCIA ,Oscar Kissanga amesema kuwa,mjadala huo unalenga kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wakina mama na vijana wa bidhaa za kilimo (mahindi ,mchele,maharage,soya,matunda na mbogamboga)ili kuongeza kiwango cha biashara ya mipakani katika bidhaa hizo .
Alisema lengo la majadiliano hayo ni kuinua vijana na kuwapa elimu, ikiwemo za kutambua na kukabiliana na vikwazo pindi wanapofanya biashara zao kwa lengo la kuwahamasisha wachangamkie fursa zilizopo kuanzia soko la ndani hadi la Afrika.
"Lengo ni kuhakikisha makundi haya yanapata fursa ya kujua biashara gani anaweza kufanya na kwa wakati gani vikwazo atakavyokutana navyo na namna ya kukabiliana navyo"
"Tujiandae kuhakikisha hili soko linalokuja tunazalisha bidhaa zenye viwango ili tuweze kuuza bidhaa na kukua kiuchumi," ameongeza
Awali, Ofisa Programu kutoka shirika lisilo la kiserikali la Aggra, Donald Mizambwa alisema mjadala huo unafanyika kupitia program ya Youth Entrepreneuship for the Future of Food and Agriculture (Yeffa) ambao wanashirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha wanaleta maendeleo kwenye sekta ya kilimo.
Alisema kupitia programu hiyo vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanaofanya biashara katika sekta ya kilimo ikiwemo wanaofanya maeneo ya mipakani kutoka mikoa 18 nchini wananufaika na program hiyo ili kutambua fursa za kiuchumi zilizopo
Alisema wameungana na Serikali na wadau wengine kuboresha mazingira ya kufanyia biashara katika mipaka ya mikoa ya Mbeya, Songwe, Kigoma, Kagera, Shinyanga, Mara na Arusha kwa kupunguza vikwazo visivyo vya kiforodha.
Alifafanua kuwa,Programu hiyo ilianza julai , 2024 katika kipindi hicho hadi sasa wameshafikia vijana 140,000 ambao wamepata zile fursa zilizopo kwenye kazi na bado kazi inaendelea huku lengo likiwa ni kufikia vijana 261,000 ambao wamepata fursa za kufanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu .
Alisema kuwa ,Shirika la AGRA ni shirika lisilo la kiserikali ambalo linashirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo katika kuhakilisha kuwa wanaleta maendeleo kwenye sekta ya kilimo .
Alisema kuanzia mwaka 2020/24 AGRA kwa kushirikiana na serikali wanatekeleza mradi unaojulikana kwa jina la EFFA mradi unaofadhiliwa na Mastercard Foundation kwa kushirikiana na AGRA pamoja na wadau wengine wa maendeleo .
“Takribani wiki tatu sasa hadi wiki nne walikuwa wanafanya midahalo pamoja na wadau wa serikali na vijana katika kuangalia ushiriki wa vijana katika sekta ya kilimo kwani mradi huo lengo lake ni kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo kwani kwenye kilimo kuna fursa mbalimbali ikiwemo biashara za mipakani hivyo kwenye mdahalo huo kuna wale vijana wanafanya biashara za mipakani lakini wengine hawafanyi ila wanatamani kufanya hizo biashara “Alisema
"Lengo ni kuona vijana wanapata fursa zilizopo sekta ya kilimo lengo mradi ni kuhakikisha asilimia 80 ni vijana wa kike kwani kwa tamaduni nyingi wanawake wanasahaulika na kuoneakana ni wa kufanya shughuli za nyumbani, wakati wanaweza kufanya shughuli za kiuchumi ndiyo maana tunawashirikisha hapa," Alisema
Mmoja wa washiriki kutoka mkoani Arusha, Vanessa Paul, amesema mafunzo hayo yatawasaidia hasa vijana wa kike kutambua zaidi fursa zilizopo na namna ya kuzitumia katika kukuza uchumi na kuondokana na utegemezi.
Tunashukuru mjadala huu umetuelimisha masuala mengi ikiwemo kutambua fursa zilizopo nje ya nchi lakini namna ya kuripoti vikwazo vya kibiashara pale tunapokutana navyo na tunaamini tukiwekeza kwenye kilimo tutakuza uchumi wetu binafsi na wa taifa kwa ujumla,"' Alisema
Ends.....
0 Comments