WANACCM WAMKERA SABAYA KAULI YA UNATUACHAJE YAMCHEFUA

By Ngilisho Tv



Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Thomas Ole Sabaya amekemea baadhi ya wanachama wao na wananchi kwa ujumla kutumia kauli ya "unaniachaje' yenye kiashiria cha kuomba Rushwa hasa katika chaguzi mbalimbali nchini.


Amesema kuwa kauli hiyo ambayo imeota mizizi, utekelezaji wake ni kutoa Rushwa kitendo ambacho haiwezi kuzalisha viongozi wenye nia ya kutumikia wananchi bali viongozi mzigo.


 Sabaya ameyasema hayo kwenye mkutano wa kuunga mkono azimio la CCM  la kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu na Dk Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar iliyofanyika jana jijini Arusha.


Katika mkutano huo ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Arusha, Sabaya amewataka wananchi kuhakikisha mwaka huu wanapingana na vitendo vya Rushwa kwa kumpitisha kiongozi ambae amekuwa akitumikia wananchi kwa weledi.


"Tusidanganywe na fedha za Rushwa kwani viongozi wanaochaguliwa na Rushwa ni jambazi na hata kesho hatakutumikia, nawaambia haya kwa sababu tabia ya kuuliza wagombea 'unatuachaje' imeota mizizi " amesema Sabaya na kuongeza


"Unapouliza hivyo nikuulize kwani unauza Nini au unauza utu wako kwa sh10,000 au 100,000?, sasa nikuambie hutapata kiongozi hapo maana mtu anayehonga sio kiongozi kwa asili ya Tanzania hivyo nyie mnaobaki mkisema unatuacheje hiyo sio kazi, katafute kazi utoe jasho ukale kwa Amani na ukapige kura yako kwa furaha" amesema Sabaya.





Awali akisoma tamko hilo, Katibu Mkuu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mussa Matoroka amesema kuwa wamefikia hatua ya kuunga mkono azimio la mkutano mkuu wa Chama hicho kutokana na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao wakuu wa nchi.


 "Sisi CCM Mkoa wa Arusha, kwa kauli moja tunaridhia azimio la mkutano mkuu uliofanyika January 18 na 19,2025 la kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais Tanzania bara na Dk Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar"amesema na kuongeza;


"Tumefikia hatua hiyo kuthamini kazi waliyofanya katika nchi hii, ambayo kwa Arusha miradi Mingi imetekelezwa ikiwemo ya Elimu, maji, barabara, utalii na nyinginezo " .


Kwa upande wake M'bunge wa Arusha mjini, Mrisho Gambo amesema kuwa yeye akiwa mmoja wa wajumbe waliompitisha Rais Samia na Dk Mwinyi wamefanya hivyo kwa kutambua kazi kubwa waliyofanya katika nchi hii lakini bado Wana kazi nyingine ya kukamilisha walichonacho.


Mimi nilikuwa mmoja wa wajumbe waliopitisha jina la Rais Samia kuwa mgombea urais kwa sababu bado ana kazi ya kufanya ukizingatia maendeleo makubwa tuliyonayo yeye amekuwa Kinara wetu, sasa nani hapendi maendeleo ya kuhakikisha huyu mkombozi anabaki ili tuendelee kufaidi? Amesema Gambo.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments