Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Arusha imetangaza kuanza kuwachukulia hatua kali wananchi wanazofanya uharibifu wa mazingira katika miti iliyopandwa kwenye barabara za njia nne wakiwemo waendesha Pikipiki na daladala wanaokatiza katikati ya barabara kinyume cha sheria.
Akiongea katika zoezi la upandaji miti katika barabara ya Arusha Moshi,lililozinduliwa na mkuu wa Mkoa, Paul Makonda, mwishoni mwa wiki,kaimu Meneja wa TANROADS Mkoani hapa,Mhandisi Christopher Saul alisema kumekuwepo ha changamoto kubwa ya utunzaji wa mazingira katika barabara za njia nne kutokana na uharibifu wa mazingira inayofanywa na wananchi.
"Leo tuna uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika barabara yetu ya Arusha-Moshi ya njia nne yenye urefu wa Kilometa 14 na miongoni mwa sera za serikali ni utunzaji na uhifadhi wa mazingira,ni jukumu letu kuhakikisha tunaunga Mkono sera hiyo na leo tunapanda miti 1200 ikiwemo Miharadai 400 na Midodoma 500 na tunawaomba wananchi tushirikiane kuitunza"
Alisema katika mkoa wa Arusha kumekuwepo na Changamoto kubwa ya wananchi kutofuata taratibu za utunzaji wa mazingira na miundo mbinu ya barabara.
"Kwa mfano katika barabara ya njia nne ya Arusha Moshi kumekuwepo na Changamoto ya watu kukatiza Katika ya barabara wakiwepo waendesha bodaboda pamoja na madereva wa haice na kufanya uharibifu wa miti na majani yaliyopandwa"Alisema na kuongeza
"Nitoe wito kwa wananchi wa jiji la Arusha kuhakikisha wanatunza mazingira na kuepuka kutupa taka ngumu yakiwemo makopo ya maji na kusababisha uchafu Katika barabara hizo tumepanga kuwachukulia hatua kali kuanzia sasa"
Pia Mhandisi Saul alikerwa na hatua ya ujenzi holela wa vibanda pamoja na uwekaji ovyo wa mabango katika barabara zake bila kufuata sheria.
Ametoa wito kwa mwananchi ama taasisi yoyote inayohitaji huduma ya mabango ama kuweka kubanda kufuata utaratibu wa kuomba kibali TANROADS.
"Kumekuwepo na tabia ya watu kuweka mabango bila kufuata taratibu, niwaombe wananchi tushirikiane katika utunzaji wa mazingira katika barabara zetu"
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Paul Makonda ameiagiza TANROADS kuhakikisha inapanda na kustawisha miti katika barabara inayotengeneza .
"Naomba nitoe agizo na hili sio ombi kwa TANROADS wahakikishe wanapanda miti katika barabara zote wanazojenga na sio kukata miti na kama wakikata miti lazima wapande miti"
Katika kampeni hiyo, Makonda amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho huku akiwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za usafi na kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi ili kusaidia kuhifadhi vyanzo vya maji na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
"Leo nina furaha kwa kwasababu tunazindua kampeni, tunapanda miti, na ninafuha kwasababu ninasherekea siku yangu ya kuzaliwa”.Alisema.
Kampeni hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali, watumishi wa umma, wanafunzi, pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Arusha, ambapo miti 1,200 imepandwa katika eneo la bustani ya barabara ya Moshi Arusha.
Aidha, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, na wananchi kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika juhudi za kutunza mazingira kwa kufanya usafi mara kwa mara na kupanda miti zaidi ili kuimarisha mazingira na kuboresha hali ya hewa.
Ends...
0 Comments