NCAA KUPELEKA WANAWAKE ZAIDI YA 800 HIFADHI YA NGORONGORO, YAPANGA KUADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE KWA KUTALII KWA BEI NDOGO!

 Na Joseph Ngilisho-ARUSHA


MAMLAKA ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imepanga kuadhimisha  siku ya Wanawake Duniani, 8 Machi 2025 inayofanyika kitaifa Mkoani Arusha,kwa kupeleka wanawake zaidi ya 800  katika hifadhi zake  ili kujionea vivutio mbalimbali.

Lengo la kutembelea hifadhi ni kujionea vivutio vingi vilivyoko katika hifadhi hiyo pia ni kujionea kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii kupitia filamu za Royal Tour na Amazing Tanzania.
 

Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo Februari 22, 2025 Kamishna msaidizi wa Uhifadhi NCAA, Mariam Kobelo alisema safari hiyo itafanyika Mach 7th, 2025 siku moja kuelekea kwenye kilele cha siku ya wanawake duniani itakayofanyika kitaifa Jijini Arusha.

Alisema kwa kushirikiana na kampuni ya utalii ya Tanzanite Cooperate, bodi ya utalii pamoja na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha wanawake watakaopata nafasi ya kusafiri kwenda hifadhini watachangia kiasi cha shilingi 170,000 ambapo fedha hiyo itatumika kulipia huduma zote muhimu.

” Tumepanga kuwapeleka wanawake wa Tanzania kutalii na kuona mambo makubwa ambayo Rais Samia ameyafanya kupitia filamu ya Royal Tour na Amazing Tanzania, watalipia kiasi kidogo cha 170,000 ambapo utapata chai ya asubuhi chakula cha mchana, kiingilio na gharama ya usafiri”



Alisema pia kwa kushirikiana na jeshi la polisi kitengo cha trafiki ulinzi umeimarishwa kuhakikisha kila mtu atakayesafiri anakuwa salama bila kupata tatizo lolote awapo safarini.

Aidha Kamishna wa uhifadhi Mariam alisema pia wanawake katika hifadhi gya Ngorongoro wamepanga kufanya usafi kwenye barabara ambazo watalii hupita kuingia katika hifadhi hiyo pamoja na kwenda hospitali kutoa misaada kwa wagonjwa.

Mkurugenzi wa kampuni ya kitalii ya Tanzanite cooperate, Eline Mwangomo alisema safari hiyo ya siku moja itaanza saa 12 asubuhi katika ofisi za Mkuu wa Mkoa kuelekea Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro na kurejea jioni Arusha.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Thabea Mollel amewahakikishia wanawake wote watakaoshiriki safari ya utalii Ngorongoro watapata usalama wa hali juu katika safari ya utalii katika hifadhi ya Ngorongoro na kurudi Arusha.

Wanawake ambao watahamasika kuunga mkono jitihada za utalii wa ndani wanaweza kupiga namba 0758171914 au Namba 0763 291179 kisha watapewa utaratibu.

Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa inafanyika mkoani Arusha na kuambatana na shughuli mbalimbali .










Ends...




Post a Comment

0 Comments