Na Joseph Ngilisho ARUSHA
KATIKA hali isiyokuwa ya Kawaida Madiwani wa halmashauri ya jiji la ARUSHA, wamejikuta wakiangua kilio kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda kugombea nafasi ya ubunge jimbo la Arusha mjini,muda utakapofika.
![]() |
Diwani wa Kata ya Themi, Lobora Petro (CCM), alieleza kwa hisia kali namna ambavyo Gambo anavyowavuruga na kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo ,akiendekeza majungu ,fitina na uchonganishi huku akiwa hashiriki vikao halali vya madiwani pamoja na kamati zake .
"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,Gambo alikuwa umekaa hapa. Huyu jamaa aliposikia unakuja alipita hapa utafikiri amechomwa moto! Maana yake uongo na ukweli vinajitenga," alisema Lobora huku akishangiliwa na madiwani wenzake.
Lobora ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Gambo aliongeza kuwa Gambo amekuwa akiwakwamisha madiwani na maendeleo ya Jiji la Arusha na kumwomba mkuu huyo wa Mkoa Makonda kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ambalo limekosa mbunge sahihi anayeweza kushirikiana na viongozi wenzake kuwaletea maendeleo wananchi.
"Tunakuhitaji kwa sababu tunataka mtu atakayeonyesha njia. Baraza hili limekwama kwa sababu ya mbunge. Mimi ninalia kwa uchungu kwa sababu ninajuta kumuunga mkono kichwa cha mwendawazimu!" alisema huku machozi yakimtoka.
"Tulikosea, tulimchagua mtu asiyejitambua! Narudia tena kukuomba msamaha kwa niaba ya wananchi wa Arusha. Tunakuhitaji na Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) aone tunakuhitaji Arusha mara mbili. Wewe si mtoto wa Arusha? Wewe si umeoa Arusha?"
Naye naibu meya wa jiji la Arusha na Diwani wa Kata ya Kimandolu, Abraham Mollel, naye pasipo kumung'unya maneno alitamka bayana kuwa baraza hilo linamhitaji Makonda akiwa mbunge na wakati ukifika alimwomba achukue fomu za kugombea.
"Watu wakisema sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Muda ukifika, chukua fomu, tuko nyuma yako! Leo umekaa hapa, Mungu akinirudisha, naomba nikae pale na wewe ukae hapa kama mbunge. Chukua hayo maneno, endelea kuyatafakari."
Madiwani waliendelea kusisitiza kuwa wanahitaji mbunge anayefanya kazi kwa vitendo na kushirikiana na viongozi wengine badala ya kuwakwamisha.
Diwani Lobora pia alimueleza Makonda kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa kiwanda kikichokufa cha kuzalisha mataili cha General Tire waliodai kunyimwa haki zao.
"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, kuna wafanyakazi wa General Tire wamenyimwa haki zao za msingi. Walitengeneza kabrasha kwa gharama ya shilingi 50,000 na nikampa mtu ambaye nilidhani angefanyia kazi, kumbe alilitupa. Badala yake akamleta waziri na kumshauri eneo hilo ligawanywe kuwa viwanja vidogo vidogo!" alisema diwani Lobora kwa uchungu.
Hata hivyo alisema aliamua kulifikisha suala hilo kwa viongozi wa juu na kufanikiwa kuondolewa madarakani kwa waziri huyo lakini bado wafanyakazi hawajapata haki zao hadi leo.
"General Tire ina wafanyakazi zaidi ya 3,000 wanaodai haki zao. Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, ukiniruhusu nitakuletea kabrasha lao na wawakilishi wao ili waone Mungu wa Makonda yupo Arusha na atawatetea na watapata haki zao," alisema diwani huyo.
Makonda aliwataka Madiwani kutokukunali fesha za umma kuwekwa mfukoni mwa walafi wachache wasiotaka maendeleo ya wananchi .
Ends...
0 Comments