Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WAJUMBE wa ccm kata ya Levolosi wilaya ya Arusha, wameonesha kutoridhishwa na uongozi wa katibu wa chama hicho katika kata hiyo ,Aisha Mubarak wakimtuhumu kwa ubadhilifu wa Mamilioni ya fedha za miradi mbalimbali ya biashara katika kata hiyo.
Wakiongea jana kwa sharti la kutotajwa majina mara baada ya kumalizika kikao cha kumsulubu kilichoketi ofisini kwake kwa zaidi ya masaa nane na kuhudhuliwa na katibu wa CCM wilaya ,Timoth Sanga madai ya wajumbe hao kutoka matawi ya Majengo na Kaloleni ni kutaka katibu huyo aondolewe wakimtuhumu kutafuna mamilioni ya fedha za miradi ya biashara.
Wajumbe walidai kuwa Katibu wao ni mbabe ,haambiliki,hashirikishi wenzake kwenye suala la ukusanyaji na matumizi ya mapato na amekuwa akipokea fedha thasilim za malipo ya kodi kinyume na utaratibu.
"Tumeandika barua ya Malalamiko juu ya katibu huyo na nakala tukapeleka kwa katibu wa CCM Wilaya,katibu wa ccm Mkoa na ccm Taifa tukiwajulisha jinsi Kiongozi huyu alivyo hafai lakini hadi leo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa "Alisema mjumbe mmoja
Kwa mujibu wa wajumbe ikiwemo kamati ya siasa ya Kata Sekretarieti ya kata na wajumbe wa halmashauri kuu ya Kata,mapato katika kata hiyo ni takribani sh,milioni tatu kwa mwezi lakini fedha hizo hazijulikani zinaenda wapi huku katibu huyo akidaiwa kutafuna fedha hicho kama mchwa na kujifanya mungu mtu kwa kutowathamini viongozi wa chini yake.
"Kuna wakati tuliomba kiasi cha sh, milioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa maduka matatu ya biashara lakini katibu alijiongezea fedha zingine na kufikia kiasi cha sh,milioni 25 ambazo alizitumia isivyojulikana na bila kushirikisha kiongozi yoyote wa chama katika kata hiyo"kilisema Chanzo Makini.
"Kana kwamba haitoshi katibu huyo amekuwa hatoi posho za wajumbe kwenye vikao,amekuwa akipokea fedha za kodi ya maduka matano na Carwash Mkononi tofauti na utaratibu wa kutumia control number na hajawahi kusoma mapato na matumizi tangu ameingia madarakani 2022"
Wajumbe hao wameingiwa na mashaka na wizi uliotokea ofisini kwake baada ya kudai ameibiwa TV ya chama, Laptop,Kompyuta na Printer Mashine wakati hapakuvunjwa na yeye ndio anashikilia funguo za ofisi Hiyo.
Pia wamemtuhumu kukamata vitu vya mpangaji aitwaye Dora vyenye thamani ya sh,milioni 7 baada ya kushindwa kulipa kodi na vitu hivyo havijulikani vilipo na alipotakiwa kuonesha alipovihifadhi alidai ufungo umepotea jambo ambalo walidai ni udanganyifu na huenda ameviuza ama amehamishia nyumbani kwake.
Baada ya wajumbe hao kumbana kuhusu fedha zinazotokana na makusanyo ya kodi alidai ana kiasi cha sh, milioni kumi na alipotakiwa kuonesha fedha zilipo alikosa majibu.
Hata hivyo wajumbe hao wamemlaumu katibu wa ccm wilaya Timothy Sanga kwa kumkumbatia kutokana na tuhuma zinazomkabili na kushindwa kutoa majibu katika kikao hicho kuhusu hatima ya katibu huyo ambaye hawamtaki na hawapo tayari kufanya naye kazi.
Katibu Sanga anadaiwa kuwabembeleza wajumbe hao kwa kuwapeleka kuwanunulia chakula huku akiwasihi waachane na jambo hilo kwa kuhofia uchaguzi hatua ambayo walisema hawapo tayari kurubuniwa ila wanachotaka katibu aondoke!
Kabla ya kikao hicho wajumbe hao walijaribu kufunga ofisi hiyo ili asiingie ndani kwa madai kwamba wamechoshwa na tabia yake isiyokoma ya ubinafsi na ubadhilifu wa mali za chama.
Hata hivyo waandishi wa habari walipomhoji katibu huyo juu ya madai hayo aligoma kuongea na kuwafukuza ofisini kwake akidai yeye sio msemaji wa chama.
Katibu wa ccm wilaya ya Arusha,Timothy Sanga alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa jambo hilo baada ya kikao hicho kumalizika ,hakuwa tayari kutoa ushirikiano badala yake aliondoka eneo hilo bila kusema chochote.
Kwa mujibu wa wajumbe hao wametishia kutompa ushirikiano kwenye kipindi cha uchaguzi wakidai hawapo tayari kufanya kazi na katibu wao na hawatatoa ushirikiano naye kwenye suala la uchaguzi iwapo ataendelea kuwepo.
Ends...
0 Comments