HOSPTALI YA RUFAA MKOA WA ARUSHA MT MERU, YATUMIA BILIONI 5.4 KUBORESHA HUDUMA ZAKE ,YAANZISHA HUDUMA ZA KISASA ZA UPASUAJI WA MATUNDU!

Na Joseph Ngilisho ARUSHA 

 

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za afya baada ya kupokea msaada wa shilingi bilioni 5.4 kutoka kwa wadau wa maendeleo. 



Fedha hizo zimetumika kununua vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo mashine za Sit Scan na vifaa vya upasuaji wa kisasa.



Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Alex Ernest, alisema lengo la uwekezaji huo ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hususan wale wenye kipato cha chini, na kupunguza gharama za matibabu.



"Fedha hizi zimetumika kununua vifaa tiba vya kisasa vitakavyosaidia kuboresha huduma, kupunguza muda wa matibabu na gharama kwa wagonjwa wasiojiweza," alisema Dkt. Ernest.



Mbali na maboresho hayo, hospitali hiyo inatarajia kuzindua huduma mpya zitakazowasaidia wananchi wengi. Moja ya huduma hizo ni upasuaji wa njia ya matundu, ambao utaanza kutolewa rasmi mwezi Oktoba 2025. 



Huduma hii itawezesha wagonjwa kufanyiwa upasuaji bila kufanyiwa michirizi mikubwa, hali itakayopunguza muda wa kulazwa hospitalini, kuongeza ufanisi wa madaktari na kupunguza madhara kwa mgonjwa.



"Huduma hii ya upasuaji kwa njia ya matundu itaanza kutolewa mwezi wa kumi mwaka 2025. Itapunguza muda wa mgonjwa kulazwa, kuongeza ufanisi wa madaktari, na kupunguza madhara ya kubaki na kovu kubwa baada ya upasuaji," alieleza Dkt. Ernest.



Pamoja na hayo, hospitali hiyo inatarajia kuanza kutoa huduma ya tiba ya saratani kufuatia ujenzi wa jengo jipya la tiba ya kemia. 

Jengo hilo limejengwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo na huduma zitaanza rasmi mwezi Mei 2025. 



Huduma hii itawezesha wananchi wa Arusha na mikoa jirani kupata tiba karibu badala ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hiyo katika hospitali za mbali.



Dkt. Ernest amesema kuwa jengo hilo limejengwa kutokana na faida zilizopatikana baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua milango ya utalii kupitia filamu ya The Royal Tour, ambayo imechangia uchumi wa mkoa wa Arusha na kusaidia kuboresha sekta ya afya.



"Jengo hili la tiba ya saratani limejengwa kutokana na faida zilizopatikana baada ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua milango ya utalii kupitia filamu ya The Royal Tour. Filamu hiyo imechangia uchumi wa mkoa wa Arusha na kusaidia kuboresha sekta ya afya," alisema.



Huduma nyingine mpya zinazotarajiwa kuanza kutolewa ni pamoja na uzalishaji wa hewa tiba, ambayo itasaidia upatikanaji wa gesi muhimu za matibabu hospitalini. Aidha, ujenzi wa jengo la damu salama umekamilika, jambo litakalohakikisha upatikanaji wa damu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo kwa haraka.



Pia, hospitali hiyo inatarajia kuanzisha huduma ya afya ya nyumbani, ambapo wagonjwa watapata huduma bila kulazimika kulazwa kwa muda mrefu hospitalini.



Dkt. Ernest amewataka wananchi wa Arusha na mikoa jirani kutumia fursa ya huduma hizi mpya, kwani zitawapunguzia gharama za matibabu na kuimarisha huduma za afya kwa wote.



"Tunawakaribisha wananchi wote kutumia huduma hizi pindi zitakapoanza rasmi. Malengo yetu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora bila kusafiri umbali mrefu," 

 Ends.....

Post a Comment

0 Comments