DR.MPANGO AAGIZA TAASISI ZOTE ZA UMMA KUJUMUISHWA NA e-GA


By Ngilisho Tv 

MAKAMU wa Rais Dk Philip Mpango ametoa rai kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kukamilisha mchakato wa kusanifu na kujenga Mfumo Mkuu wa Ubadilishanaji Taarifa Serikalini na kuhakikisha Taasisi zote za umma zinajumuishwa katika mfumo huo.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Tano cha Mamlaka ya Serikali Mtandao kinachofanyika jijini Arusha.


Amesema jambo hilo ni muhimu ili kurahisisha utendaji kazi katika taasisi na kurahisisha utoaji huduma kwa wananchi kama ilivyoelekezwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa taasisi za umma kuhakikisha kuwa mifumo yao inasomana na kubadilishana .


Aidha Makamu wa Rais amesema taasisi zote za umma zinapaswa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao katika hatua zote za ujenzi au ununuzi, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya TEHAMA pamoja na kuwataka kuwaelekeza wakuu wote wa taasisi za umma kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Mamlaka husika katika utekelezaji wa shughuli za Serikali Mtandao.


Hali kadhalika, Makamu wa Rais ameagiza mikoa ambayo bado haijaanza kutumia utaratibu wa Ofisi ya Kielektroniki (e-office) kuhakikisha wanaaanza kutumia mfumo huo ifikapo Juni 30. Aidha ameagiza kituo cha utafiti kiweze kuimarishwa pamoja na kuongezewa eneo la ufanyaji kazi.


Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA na kada nyingine, kwa kuweka mazingira wezeshi ya ufundishaji katika Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu ili viendelee kuzalisha wataalam wa kutosha.


Dk Mpango amewasihi washiriki wa kikao kazi hicho pamoja na Watanzania wote kwa ujumla, ambao wana sifa za kupiga kura, kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuhakikisha wanajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura ili kuchagua viongozi wenye sifa na uwezo stahiki wa kusimamia na kuratibu shughuli za maendeleo katika ngazi husika.

Post a Comment

0 Comments