DKT. BITEKO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI INDIA,AMPONGEZA ANISA KWA KUZANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI NCHINI

 By Ngilisho Tv 


DKT. BITEKO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI INDIA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametembelea Ubalozi wa Tanzania nchini India na kuzungumza na Watumishi katika ofisi hiyo.


Akizungumza katika Ofisi hizo  jijini New Delhi, Dkt. Biteko amempongeza  Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega kwa mapokezi mazuri na kazi nzuri  zinazofanywa na Ubalozi huo ikiwemo kutangaza fursa za uwekezaji.



“ Nakushukuru kwa mapokezi mazuri mliyotupatia tangu tulipofika hapa kwa kweli  yamerahisisha utekelezaji wa  majukumu yetu, mnaipa heshima kubwa Serikali kwa namna ambavyo Ofisi hii  inavyohudumia watu mbalimbali wenye uhitaji wanapokuja hapa ikiwemo watu wanaoonesha nia ya kuwekeza Tanzania au Watanzania wanaotaka kuwekeza hapa India." Amesema Dkt. Biteko


 Amesema ushiriki wa Wizara ya Nishati katika Mkutano wa Wiki ya Nishati India umekuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kuhamasisha ushiriki wa wawekezaji mbalimbali katika duru ya tano ya kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia.


Ameongeza kuwa " Kwa upande wa Wizara ya Nishati tutajitahidi watu wanapotoka India kuja Tanzania kama wawekezaji tuwape ushirikiano mzuri,” 


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Iddi Kassim amesema Kamati hiyo imefarijika kwa kupata fursa ya kushiriki Wiki ya Nishati nchini India ambapo wamejifunza masuala mbalimbali na kupata uzoefu katika usimamizi wa sekta  ya nishati hasa ikitambulika kuwa India imepiga hatua kubwa kwenye nishati.


Dkt. Biteko amemaliza ziara yake ya siku tano nchini humo ambapo anarejea nchini Februari 15, 2025.


Awali, Balozi wa Tanzania  nchini India, Mhe. Anisa Mbegai alimshukuru Dkt. Biteko kwa ziara ambayo amesema kuwa imewaheshimisha kama wenyeji wa Ujumbe wa Tanzania nchini India.


" Nitumie fursa hii kukupongeza kwa majukumu yako uliyotekeleza ukiwa hapa na tunakushukuru kwa heshima kubwa uliyotupatia.” Amesema Mbega


Aidha, Mhe. Mbega ametaja baadhi ya majukumu ya Ofisi ya Ubalozi kuwa ni kuimarisha uhusiano baina ya nchi za uwakilishi, kulinda maslahi ya nchi na kuhakikisha fursa mbalimbali zinapatikana kama vile masoko, utalii na uwekezaji.




📸:Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Post a Comment

0 Comments