By Ngilisho Tv
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imemuhukumu mfanyabiashara Khamis Luwonga (38), anayetuhumiwa kumuua mkewe Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kuua kwa makusudi.
Hukumu hiyo imesomwa leo na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama hiyo baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha shaka lolote na huku ikieleza kwamba katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa alichokieleza ni kweli kwamba alimuua mke wake na kisha kumchoma moto.
Hata hivyo, mshtakiwa baada ya kutiwa hatiani na mawakili wa pande zote mbili kuzungumza mshtakiwa alitaka kuzungumza, Jaji Mwanga alikataa na kumueleza asubiri kwanza lakini alikaidi ndipo Jaji akaita askari kumtuliza ili aendelee na kutoa adhabu.
Jaji Mwanga amesema hilo ni kosa la mauaji mikono yake imefungwa kiapo chake cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sheria za Tanzania adhabu ni moja tu kunyongwa hadi kufa.
"Nina muhukumu Khamis Luwonga maarufu kwa jina la Meshack adhabu ya kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake Naomi Marijani," amesema Jaji Mwanga
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mwandamizi Ashura Mnzava ameiomba Mahakama iwapatie mabaki ya mwili wa Naomi ambayo yalitolewa kama kielelezo, ambapo ndugu wameomba wakayazike mabaki hayo kwa sababu hawakuwahi kufanya mazishi ya mpendwa wao.
Ndugu wa marehemu, Robert Marijani akiwa nje ya Mahakama amesema watakwenda kuzika mabaki hayo ili kumpuzisha ndugu yao mpendwa ambae hakuwahi kuzikiwa tangu umaiti wake.
Pia, ndugu jamaa na marafiki wameshindwa kuzuia hisia zao na kuanza kulia kwa uchungu wakisema hadi haki imepatikana ndugu yao atapumzika kwa amani.
Katika kesi hiyo ya muaji namba 44 ya mwaka 2019, mshtakiwa Luwonga ambaye ni Mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa Mei 15, 2019 akiwa Gezaulole eneo la Kigamboni alimuua Naomi Marijani.
0 Comments