Na Joseph Ngilisho ARUSHA
FAMILI tatu za jamii ya kifugaji wa kimasai wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha ,wamemwomba waziri wa maendeleo ya jamii jinsia wanawake na wenye makundi maalumu, Dorothy Gwajima kuwasaidia kupatikana kwa watoto wao watatu waliochukuliwa kwa madai ya kupatiwa ufadhili wa masomo na kutoonekana kwa zaidi ya miaka 10 tangu 2015.
Aidha wazazi hao ambao wametokea kitongoji cha Olobo kilichopo kijiji cha Lopolun kata ya Olorien na Magaiduru katika tarafa ya Loliondo wilayani humo, walidai hawajui kama watoto wao wapo hai ama wamekufa ila wanasikia wapo mkoani Arusha na wamebadilishwa majina yao ya asili na kupewa majina ya kiislamu.
Wazazi hao wanamtuhumu afisa ustawi wa jamii wilayani humo , kufanikisha mpango huo wa kuchukuliwa kwa watoto wao wa kike na pindi wanapomuuliza ni wapi walipo watoto wao amekuwa hatoi ushirikiano .
Wakizungumza na waandishi wa katika ofisi za shirika la kutetea haki za wanawake na watoto la MIMUTIE WOMEN ORGANIZATION lililopo mkoani Arusha ,wazazi hao ambao ni Nalangu Koila ,Naramat Ngai,na Leyaley Salangat wamesema kuwa, mwaka 2015 watoto wao watatu wa kike wanaojulikana kwa majina ya Seyo Koila,Kitindi Ngai na Timbiyani Salangati wakiwa na miaka mitano, walichukuliwa chini ya usimamizi wa afisa ustawi wa jamii wilaya ya Ngorongoro anayejulikana kwa jina la Benezeth Bwikizo .
Wamesema kuwa,watoto hao walichukuliwa kwa taarifa kwamba wanakwenda kupatiwa ufadhili wa kusomeshwa na wakati watoto hao wanachukuliwa mwaka huo walikuwa na umri wa miaka mitano na hadi sasa watoto hawajarudishwa kwa wazazi wao na wala wazazi wao hawana taarifa ya mahali walipo.
"Tangia watoto hawa wanachukuliwa sisi tulikuwa hatujui wanapelekwa sehemu gani,kwani alikuja mtu mmoja aitwaye Mepukori ambaye kwa mwaka huo alikuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Oloboo na ndiye alieenda kwa wazazi wa watoto hao na kudai kuwa ameagizwa na Afisa ustawi wa jamii wilaya ya Ngorongoro Benezeth Bwikizo aje kutafuta watoto ambao hawana uwezo ili wasaidiwe. "alisema.
Aidha wamesema kuwa, Mepukori ndiye aliyechukua watoto hao mikononi kwa wazazi wao na kuwapeleka kwa Benezeti ambaye alibadili taarifa zao na kuwaandikisha kama watoto yatima , na wazazi walipouliza kuhusu watoto wao hawakupewa taarifa yeyote ya mahala walipo na mtu ambaye aliwachukua watoto hao kwa wakati huo.
"Wakati watoto hao wanachukuliwa na kusafirishwa siyo ndugu wa watoto au wazazi wa watoto waliyejua ni wapi walikuwa wanapelekwa ila waliambiwa wamepata mfadhili wa kuwasomesha bure na wangerejeshwa baada ya masomo lakini hadi sasa miaka 10 imepita hawajawahi kuwaona "
Aidha baadaye wazazi walipohoji kuhusu mahali Benezeti alipowapeleka watoto wao, Benezeti aliwaambia wazazi hao wawasiliane na mtu ambaye yupo na watoto, mtu ambaye wazazi hao walikuwa hawamfahamu kwa wakati huo.
Hata hivyo wazazi hao wamesema kuwa,baadaye mwaka 2021 mwenyekiti mpya wa kitongoji cha Oloboo,Kimati Tooko alifuatilia suala hili baada ya wanakijiji wengine kuja juu wakitaka watoto hao warejeshwe makwao ndipo Benezeth alipomkutanisha mwenyekiti huyo katika ofisi ya ustawi wa jamii iliyopo katika hospitali ya Mount Meru Mkoani Arusha na kuoneshwa aliyewachukua watoto hao na mwenyekiti aliweza kumwona ila hakutakiwa kuwaona watoto wala kuzungumza nao .
Wakati huo huo ,Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake la MIMUTIE WOMEN ORGANIZATION limeingilia kati sakata la kupotea kwa watoto hao baada ya kupata taarifa ya kuchukuliwa kwa watoto hao katika mazingira ya kutatanisha .
Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo ,Rose Njillo amesema kuwa, waliamua kufuatilia kwa huyo Afisa ustawi wa jamii wa wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bwikizo anayetajwa kufanikisha mpango huo ambapo alisema ni kweli kuwa watoto hao wamechukuliwa lakini aligoma kutoa ukweli wa taratibu za kisheria zilizotumika kuwachukua watoto hao na pia aligoma kutoa taarifa inayoonyesha jinsi watoto hao walivyochukuliwa na kusema taarifa hiyo anaweza kuitoa mahakamani pekee yake.
"Pia baada ya Benezeth kuulizwa zaidi ,alisema kuwa suala hili litaendelea kufuatiliwa, basi atasimamisha ufadhili wa watoto hao ,na kusema kama mnataka kuwarudisha hao watoto je mnaweza kurudisha gharama zilizotumika kuwatunza hao watoto "alisema Bwikizo.
Aidha Mkurugenzi huyo alisema kuwa,wao kama wanaharakati wa masuala ya ulinzi na usalama wa watoto ,wanaamini kwamba watoto wana haki ya kuwaona wazazi wao hata kama waliishi katika mazingira magumu na wazazi wana haki ya kuwaona watoto wao.
Watetezi hao wamemwomba Waziri Gwanyima kuingilia kati na kuwachukulia hatua wote waliohusika kuwachukua watoto hao wa jamii ya kimasai bila idhini ya wazazi wao kwa lengo la kujinufaisha,huku wakilitaka jeshi la Polisi kuingilia kati na kuchukua hatua kwa wale waliobainika kushiriki mpango wa kuchukua watoto hao na kuwapeleka kusikojulikana.
Ambapo amesema wahusika wa tukio hilo hawana tofauti na watu wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu .
Kwa upande wa Afisa ustawi wa jamii akihojiwa na waandishi wa habari kwa njia ya simu juu ya tuhuma hizo alisema hawezi kuzngumzia sula hilo hadi atakapopewa idhini ya kuzungumzia na bosi wake ambaye hakumweka bayana ni yupi.
"Siwezi kuzungumzia suala hilo.kwani mimi.sio.msemaji hadi nitakapopewa idhini na mkuu wangu wa kazi ."alisema Benezeth Bwikizo.
Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Olaboo ,Kimati Tooko,alisema alisema watoto hao walichukuliwa kwa wazazi hao kwa lengo la kusaidiwa kusomeshwa kwa madai kwamba wazazi hao hawana uwezo wa kuwasomesha.
"Wakati wanachukuliwa wazazi wao waliambiwa wanaenda kusomeshwa na mfadhili ila hadi leo miaka zaidi ya 10 hatujawaona hao watoto ila nasikia wapo Arusha"
Ends....
0 Comments