DOKTA MAYALA ATOA MUAROBAINI WA KUYAEPUKA MAGONJWA HATARI
Na Lydia Lugakila
Bukoba
Jamii Mkoani Kagera imehimizwa kutumia vyakula vya asili ili kuepuka magonjwa mbali mbali yakiwemo yanayojitokeza kwa wingi kwa nyakati hizi.
Kauli hiyo imetolewa na Daktari John Mayala kutoka zahanati ya St. John iliyopo Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake
Dokta Mayala amesema kuwa jamii ya sasa imepuuza kutumia vyakula vya asili hali iliyosababisha mtu kupata magonjwa mbali mbali yakiwemo ya sukari, maumivu ya viungo kansa, presha na mengine mengi.
Amesema kuwa mwili wa Binadamu unajengwa na seli mbali mbali ambapo kila seli ina kazi yake na kuwa kila seli utengeneza kitu kiitwacho Radicals ambao ni uchafu unaotengenezwa kwenye seli
Amesema kuwa Radicals nyingi zinatengenezwa kutokana na kutokutumia vyakula vya asili ikiwemo karoti, mboga za majani, matunda kwani hivyo ni vyakula muhimu Katika kujenga mwili ambapo pia ameongeza kuwa miili ya mwanadamu inashambuliwa sana na magonjwa huku tatizo likiwa ni kupuuza vyakula vya asili.
"Radicals zinapokuwa nyingi katika mwili wa binadamu zina madhara zikibadilika ndo maana mtu hupata maumivu kama ya kuchomwa chomwa na vitu mwilini hivyo mwili unahitaji Anti- oxidants ambazo ni kemikali zinazozalishwa sehemu mbali mbali za mwili na kazi yake ni kuondoa sumu mwilini" alisema Dokta Mayala.
Aliongeza kuwa ubichi wa vyakula ikiwemo kabichi, nyanya, vitunguu, karoti na vinginevyo vyenye kujenga mwili vina utajiri mkubwa wa kutengeneza mwili vizuri kuliko vilivyopikwa kwani vya kupikwa vinakuwa tayari vimepoteza virutubisho muhimu.
Dokta Mayala alivitaja vyakula vilivyobeba Anti-oxidant kwa wingi kuwa ni vya vitamini A-C-E na D kwani husaidia kuleta Anti-oxidant mwilini.
Amesema vitamini A inabeba karoti kwa wingi mboga za majani, mayai matango,tikitimaji na parachichi na C- hubeba matunda yakiwemo tufaa, nanasi, limao na E hubeba karanga, machungwa, nyanya, mafuta ya mmea, machenza, maembe, papai na mboga za majani.
Aidha Amesema radicals zinapokuwa nyingi mwilini huleta madhara ikiwemo kansa, kusababisha kuzeeka haraka kabla ya umri, magonjwa ya ngozi huku akiongeza kuwa wavutaji wa sigara wanatengeneza Radicals nyingi mwili mwao na hawajui kuwa sigara ni chanzo cha kansa.
Ameongeza kuwa pia watumiaji wa pombe kali aina ya spirits nao wanatengeneza Radicals kwa wingi, na mtu anapougua, kuvuta hewa chafu, kula mafuta mengi husababisha uwepo wa Radicals nyingi mwilini.
Hata hivyo aliitaka jamii Mkoani Kagera kuendeleza vyakula vya asili ili kujiepusha na magonjwa yanayowagharimu kiasi kikubwa cha fedha huku akiwahimiza kupima Afya zao inapobidi ili kuyaepuka magonjwa mbali mbali.
0 Comments