By Ngilisho Tv ARUSHA
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka sh. trilioni 22.2 mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia sh. tril. 27.6 mwaka wa fedha 2023/2024 na kuvunja rekodi ya kukusanya sh. trilioni 16.528 katika kipindi cha Nusu Mwaka wa Fedha 2024/2025 kinachoanzia Julai hadi Desemba Mwaka 2024.
Aidha dkt Nchemba ameitaka TRA kuongeza ubunifu ili kupata walipa kodi wengi zaidi.
Dkt. Nchemba alitoa pongezi hizo, wakati akifungua Kikao Kazi cha siku 5 kinacho Tathmini Utendaji kazi wa Nusu Mwaka wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, kinachofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC), Jijini Arusha.
Alisema kuwa fedha hizo zimeisaidia Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati inayolenga kuboresha huduma za jamii kama vile Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere, Mradi wa Treni iendayo kasi (SGR), miundombinu ya barabara, huduma za jamii na mingine mengi
Dkt. Nchemba aliitaka TRA kuimarisha zaidi mifumo ya kisasa ya kielektroniki ya kukusanya mapato ya Serikali ili kuongeza uwazi, tija na ufanisi kwa kukusanya mapato pamoja na kuziba mianya ya maafisa wa TRA kukutana uso kwa uso na walipakodi.
Aidha, Dkt. Nchemba alirejea wito wake kwa Mamlaka hiyo kutofunga biashara za watu wanaowadai kodi badala yake waweke utaratibu wa kuzilea biashara hizo huku wakihakikisha kodi stahiki zinalipwa na wahusika kwa kuwa vitendo vya kufunga biashara vinaathiri uchumi wa nchi pamoja na kuvuruga mfumo wa biashara husika na kuwasababishia watu umasikini na kuwakosesha wananchi ajira.
Dkt. Nchemba alitumia wasaa huo pia kuwataka wafanyabiashara kuacha tabia ya kukwepa kulipa kodi, kutumia ipasavyo mashine za kukusanya mapato ya Serikali (EFDs) na kuwahimiza watoe risiti halali zinazoendana na thamani ya manunuzi yaliyofanyika huku wananchi kwa upande wao wakihimizwa kudai risiti halali wanaponunua bidhaa na huduma mbalimbali.
Aliwahimiza watumishi wa TRA kuendelea kufanyakazi kwa bidii, juhudi na maarifa ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kukusanya mapato yake kupitia kodi mbalimbali pamoja na kuzingatia weledi wanapotekeleza majukumu yao wakati Serikali kwa upande wake ikiendelea kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyakazi.
Ends ....
0 Comments