By Ngilisho Tv-
Mgombea nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu amesema chama hicho kimepoteza imani na mvuto kwa wafuasi wake wengi na wananchi kwa ujumla kwasababu ya uongozi wa sasa kuwa karibu na chama tawala na mamlaka kwa ujumla.
Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa sasa, amesema njia pekee ya kurudisha Imani na kutegemewa na wananchi ni kwa kupata uongozi mpya utaobadilisha mwelekeo wa chama hicho.
"Unasema huyu Rais hana shida yoyote. Halafu, huku wanachama wako wanatekwa nyara na kuuawa.
Na kwasababu umeshasema Rais hana shida yoyote, ni mapendano, ni raha tupu, unamwambia mwananchi gani aandamane kwasababu Mzee Ali Kibao ameuwawa, halafu akufuate? Alihoji Lissu katika mahojiano maalaum yaliyofanyika nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam.
Chadema kinatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wake wa ngazi ya taifa ndani ya wiki mbili zijazo, ambapo tarehe 21 Januari, huku nafasi ya Mwenyekiti wa chama ikigombaniwa na watu wanne; Freeman Mbowe, Tundu Lissu, Odero Charles Odero na Romanus Mapunda.
Hata hivyo mchuano umekuwa mkali zaidi kati ya Lissu na Mbowe ambapo wafuasi wao, hasa katika mitandao ya kijamii, wamebadilishana maneno na shutma mbalimbali.
Lissu amemshutumu Mbowe kwa kubadilika na kulegeza misimamo yake dhidi ya chama tawala na mamlaka kwa ujumla, akidai mabadiliko ya Mbowe yalianza kuonekana mara tu baada ya kutoka gerezani.
"Mwenyekiti aliyeenda gerezani, si mwenyekiti aliyetoka gerezani miezi minane baadae. Yule aliyetoka gerezani alikuwa tofauti, akiimba maridhiano anaimba mapendano" amesema Lissu.
Hata hivyo Mbowe ametupilia mbali shutuma zinazoelekezwa dhidi yake binafsi na chama pia akisema kwamba hazikuwa na Ushahidi wowote ule.
"Hakuna shutuma hata moja anayoileza hadharani dhidi yangu ambayo ni ya kweli, na tumeshamtaka kwamba kama una shutuma au lawama yoyote dhidi ya mwenyekiti, ilete kwenye vikao vya chama vizungumzwe" alisema Mbowe alipokuwa akizungumza na Crown Media mapema wiki hii.
Mbowe ameelezea utoaji wa kashfa na matusi vinavyoendelea katika uchaguzi wa chama chao kama utovu wa nidhamu akiongeza kwamba anatumaini uongozi mpya utakao ingia madarakani baada ya uchaguzi utashughulikia hali hiyo kwa nguvu kubwa.
Lissu ameiambia BBC kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo ya juu ya chama akiwa na malengo ya kuleta uelekeo mpya wa chama unaoongozwa na misimamo ya mageuzi.
"Hapatakuwa tena na kuimbiana maridhiano yasiyokuwepo, hakuna tena biashara ya kualikana kwenye vikao kwenda kuzungumza mambo yasiyojulikana, ni mapambano ya Kwenda kudai mabadiliko ya msingi ya nchi yetu, na itakuwa ni mapambano ya mshikemshike kweli kweli" amesema Lissu.
Makamu Mwenyekiti huyu ameuelezea uhusiano wake na Mbowe kwa sasa kuwa dhaifu.
"Tukikutana hivi, hatupigani ngumi. Lakini uhusiano haupo kama mwanzoni" amesema Lissu.
Pamoja na mvutano mkubwa unaoendelea hivi sasa kuelekea uchaguzi, Lissu amewanukuu wafuasi wa Mbowe waliosema kwamba "hakuna kuhama."
Kuhusu tishio la Chadema kuvunjika baada ya kuchaguzi kutokana na mvutano wa kampeni, Lissu amesema uimara wa chama utaendelea kubaki kama ulivyo, utategemea uchaguzi huru na wa haki utakaofanyika tarehe 21 Januari.
"Tukiwa na uchaguzi wenye mizengwe, wanachama wetu wataona, na chama hakitakuwa sana" ametahadharisha Lissu.
0 Comments