By Ngilisho Tv-Dodoma.
Chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha azimio la kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu baada y awajumbe 1924 wa mkutano Mkuu kupiga kura zote za ndio sawa na asilimia 100
Azimio hilo limepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia chama hicho. Chama hicho pia kimempitisha Dkt. Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar.
Uamuzi huo umefanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake. Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara) ambapo mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira alipitishwa kushika wadhifa huo jana Jumamosi.
Hii leo, baadhi ya wajumbe waliokuwa wakitoa michango yao juu ya utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM walipendekeza mkutano huo kuwapitisha Rais Samia na Rais Mwinyi kama wagombea wa urais kutokana na maendelea walioyasimamia.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akizungumza kama mmoja wa wazee wa chama, alisisitiza kuwa CCM ina mamlaka ya kujichagulia mgombea wao kwa wakati wowote. "Hili lipo ndani ya uwezo wetu, kuamua muda wowote, kwamfano wenzetu (wa Swapo) Namibia wao wanafanya uchaguzi kumpitisha mgombea wao mwaka mzima (kabla ya uchaguzi). Sasa na sisi tunaweza kuamua. Jambo la Msingi azimio lipite na tupate ushauri wakisheria ili uendane na matakwa ya tume ya uchaguzi."
Hii ni mara ya kwanza kwa CCM kupitisha wagombea wa nafasi za urais mapema katika mwanzo wa mwaka na katika kikao ambacho ajenda yake mahsusi haikuwa hiyo. Kawaida, maamuzi hayo hufanyika miezi michache kabla ya kuanza kwa kampeni rasmi za uchaguzi mkuu.
Hatua hii inaandika historia ya chama hicho kikongwe kwa mara ya kwanza kumsimamisha mgombea mwanamke katika nafasi ya urais.
Marais wote wawili Samia na Mwinyi wanamaliza awamu zao za kwanza za uongozi mwaka huu. Na kwa mujibu wa utamaduni wa chama hicho, marais walio madarakani huwa hawapatiwi ushindani katika kupewa tiketi ya kugombea urais kwa awamu ya pili.
Rais Samia aliingia madarakani mwezi Machi 2021 mara baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Aliingia madarakani kwa mujibu wa katiba akiwa ndiye mrithi wa urais, kwa nafasi aliyokuwa nayo kipindi hicho ya Makamu wa Rais.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kwa kuwa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu toka kufariki kwa Magufuli basi kipindi hiki kinahesabika kama muhula wake kamili na ataruhusiwa kugombea urais mara moja tu.
"Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu," inaeleza katiba ya Tanzania.
0 Comments