By Ngilisho Tv-Dar Es Salaam
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linashikilia kundi la watu wanane wanaotuhumiwa kula njama na kufanya tukio la kumteka Deogratius Tarimo.
Tukio hilo lilitokea Novemba 11, mwaka huu, eneo la Kiluvya, Ubungo, Dar es Salaam, ambapo kupitia video fupi iliyosambaa mtandaoni, ilionesha namna watuhumiwa wakimlazimisha Tarimo kuingia katika gari ndogo, huku wananchi wakishuhudia.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, akizungumzia jana kuhusu operesheni maalum ya kuzuia vitendo vya uhalifu waliyofanya, alisema wanawashikilia watu wanane katika tukio hilo.
“Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limekamata kundi la wahalifu wanane wanaotuhumiwa kula njama kwa pamoja na baadaye kufanya tukio la kumteka Deogratius Tarimo.
“Watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti Dar es Salaam, Songea, Ruvuma na eneo la Mbingu Mlimba, Morogoro. Limepatikana gari aina ya Toyota Raum ambayo lilitumika wakati wa tukio hilo,” alisema.
Kamanda Muliro alisema wakati wa tukio hilo, gari hilo liliwekwa namba isiyo halisi T 237 EGE na baada ya ufuatiliaji wamebaini namba yake halisi ni T 237 ECF.
Aliwataja watuhumiwa hao ni Bato Tweve (32), bondia (32) mkazi wa Kimara Bunyokwa, Yusuph Abdalla (32) mkazi wa Mbingu, Mlimba, Morogoro, Fredrick Juma (31) mkazi wa Kibamba, Dar es Salaam na Nelson Elimusa (24) maarufu msela dereva teksi, mkazi wa Mbezi Luguluni.
Wengine ni Benk Mwakalebela (40) maarufu tall mkazi wa Mbezi Makabe, Lusungo, Mbeya, Thomas Mwakagile (45) maarufu baba mage mkazi wa Bunyokwa, Mbeya, Anitha Temba (27) mkazi wa Mbezi Mwisho na Isack Mwaifani maarufu boxer mkazi wa Kimara Temboni Salanga.
Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi linaendelea na kazi ya kuzuia vitendo vya kihalifu, pia kuwakamata na kutokuwa na huruma kwa watuhumiwa wote wanaojihusisha na matukio ya uhalifu.
0 Comments