WAHITIMU ATC WATAKIWA KUTUMIA UBORA WA ELIMU WALIOIPATA KUPANUA SOKO LA AJIRA NDANI NA NJE YA NCHI

  Na Joseph Ngilisho, Arusha 


WAHITIMU  katika Chuo cha  Ufundi Arusha (ATC)  wametakiwa  kutobweteka wakisubiri ajira za serikalini bali watafute ajira mbadala ya kujiajiri ndani na nje ya nchi ili kupanua soko la ajira hususani katika  nchi za jumuiya ya Afrika mashariki kutokana na ubora wa elimu walioipata .



Aidha wametakiwa kuitumia  elimu hiyo kwa ufanisi ,sambamba na  kuwa waadilifu, wazalendo, wachapa kazi na kuheshimu dhamana watakayopewa kwani  ni wajibu wao kutumia taaluma zao  kutoa huduma kwa jamii . 


Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu mkuu Wizara ya Elimu, Prof Daniel Mushi,wakati wa mahafali ya 16 ya Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) ambapo wanachuo wapatao, 1,139  wakiwemo  wanawake 253 wamehitimu kozi katika ngazi mbalimbali zikiwemo Stashahada, Astashahada na Shahada .


“Ningependa kuwapongeza Wahitimu wote ambao leo hii mnatunukiwa vyeti vya kuhitimu.  Ninategemea kuwa nyie Wahitimu wa Ufundi stadi, ufundi Sanifu na Uhandisi  bila shaka mnatambua hazina kubwa ya Elimu mliyoipata.” 


Alisema kuwa Wizara inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hicho katika kutoa wataalamu ,kama Wizara inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya Ujenzi wa majengo yake kwa kutumia wataalamu kutoka chuoni hapo kutokana utaalamu wao mkubwa na Wizara imeboresha mitaala ili kuwezesha wahitimu kwenda kwenye Soko la ajira.


Prof Mushi,alisema kuwa Mahafali hayo  yawe ni chachu na fursa ya ajira na maendeleo na dunia inakoelekea ni kujijenga zaidi kwenye ujuzi na Ufundi hivyo ni wajibu wao wahitimu hao kutumia taaluma zao kuihudumia Jamii na nchi yetu haiwezi kubakia nyuma katika matumizi ya teknolojia hivyo Ufundi unahitaka sana katika maendeleo ya uchumi nchi.


"Nimeridhishwa pia na juhudi mnazofanya hapa Chuoni kupanua udahili ili kupata Mafundi Sanifu wengi huu ni mchango mzuri katika kujenga uchumi wa nchi.  Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono dhamira yenu ya kuongeza Programu Mpya na Udahili hasa katika ngazi ya Ufundi Sanifu".


"Changamoto ambayo iko mbele yenu Bodi na Menejimenti ya Chuo ni kuendelea kuboresha Mitaala ili iendane na mahitaji ya soko la viwanda.  Mitaala hiyo ilenge kutoa Elimu Bora inayowapa Wahitimu uwezo wa kushindana katika Soko la ajira au kujiajiri ndani na nje ya Nchi hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na mataifa mengine"Alisema.

                                 

Awali Mkuu wa Chuo cha Ufundi,Arusha,dkt Mussa Chacha,alisema Chuo hicho ,kimejenga tawi jipya Kijiji cha Kikuletwa Wilayani Hai mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kuwaandaa Vijana wa nchi za Afrika mashariki kwa mafunzo ya Nishati Jadidifu .


Aliongeza kuwa,chuo kinakamilisha Ujenzi wa Hospitali iliyopo ndani ya eneo la Chuo hicho ambayo itaanza kutoa huduma ya matibabu kwa wanachuo na Wananchi mwezi Machi mwakani.


Alisema kuwa Chuo hicho kimetekeleza maelekezo ya Rais ya kutengeneza mita za Maji za malipo kabla ili kuondoa malalamiko ya wateja wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Jijini Arusha,AUWSA ya kubambikiwa Ankara.


Dkt Chacha alifafanua  kuwa Chuo hicho kilizalisha mita 100, za majaribio na wamekubaliana na AUWSA kuanza kuzalisha mita hizo pia Chuo hicho linatoa ushauri wa kitaalamu kwa wanaojenga majengo ya kudumu.


Kwa upande wake  Mwenyekiti wa bodi ya Chuo cha ufundi Arusha ,Dkt.Noel Mbonde ali sema kuwa,chuo hicho kimekuwa kikifanya  vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaandaa wanafunzi kuweza kujiajiri katika nafasi mbalimbali kutokana na mafunzo ambayo wamekuwa wakifundishwa kwa vitendo.








Ends.....


Post a Comment

0 Comments