WAFUGAJI MISENYI WAMPONGEZA RAIS SAMIA

 Wafugaji wa Ng'ombe Misenyi wampongeza Rais Samia kwa mradi wa kopa Ng'ombe lipa Maziwa.

Akina Mama na vijana watakiwa kujikwamua kiuchumi.

Na Lydia Lugakila

Misenyi


Mwenyekiti wa wafugaji wa Ng'ombe katika Kijiji cha Bubale kata kakunyu Wilayani Misenyi mkoani Kagera Bi Amina Ayubu amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya wana ushirika wenzake kutokana na uwezeshaji wa mradi wa kopa ng'ombe lipa maziwa alivyoubadilisha na kuleta unafuu kwa Watanzania hasa Wana Misenyi.


Bi Amina alitoa kauli hiyo aliposhiriki siku ya maendeleo ya kata Bugandika (Bugandika day) ambapo alipata muda wa kushiriki maendeleo kwa kuahidi kiasi cha shilingi Milioni1 kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kuleta maendeleo.


Alisema kuwa jitihada za Rais Samia ni kubwa sana kutokana na kubadilisha taratibu katika ufugaji wa Ng'ombe ambapo kwa sasa hakuna Mwananchi wa kawaida kumpa Ng'ombe, alafu kesho yake ukaja kumnyanganya badala yake unampa Ng'ombe anakulipa maziwa jambo alilolitaja kuwa limewapa ahueni ya maisha.


Ameongeza kuwa Rais Samia amefungua milango yote pembezoni mwa Nchi na fursa zimejaa hivyo kila Mwananchi ajipange kufaidi matunda ya Rais Samia kwani ni Mama mchapa kazi  kwa ajili ya manufaa ya watanzania.


Akielezea mradi wa kopa Ng'ombe lipa maziwa amesema lipo shirika la umoja wa kimataifa wa uwezeshaji lijulikanalo kama international Association for Facilitators -IAF wakishirikiana na watu wa benki ya kilimo ambao walikuja na kuwahamasisha  Wanawake na Wanaume na kukubali kujiunga.


Alisema kupitia mradi huo unakopeshwa Ng'ombe unalipa maziwa ambapo hadi sasa amesaini  mkataba na msindikaji Kahama Fresh ambaye pia ndiye mzabuni wao.


"Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo  makubwa Nchi nzima  hivyo hatuna budi kuzidi kumuombea Rais wetu ili azidi kutufungulia milango zaidi"alisema Mwenyekiti huyo.


Bi Amina Ayubu alitumia fursa hiyo kuwaomba Wanawake na vijana Wilayani Misenyi kutobweteka kwani wanatakiwa kuelewa kuwa ufugaji ni fursa huku wakizingatia kuwa maisha ya sasa si mepesi.


"Wanawake tuamke najua ukiwa unavuna maziwa yako kwa siku unapata shilingi elfu 5 hadi elfu 10 watoto watasoma kila na kitu kitawezekana.


Ameongeza kuwa walisaini mkataba tangu Mwaka 2021 ambapo hadi sasa wapo wana ushirika wapatao 56 na wanatarajia kuboresha mradi huo kwa kuwa na kituo cha kupokelea maziwa kwani hadi sasa wanayasafirisha kutoka Bubale kwenda Bunazi ilipo ofisi ya msindikaji.


Aidha alisema wanajipanga kuwa na Ofisi yao na kuwa ujenzi wake umefikia hatua ya kupaua na ifikapo Januari 10,2025 wataanza kupokea maziwa ndani ya Kijiji cha Bubale ambapo pia Mkurugenzi wa shirika la AFI anatarajia kufika  kukagua jengo hilo ifikapo Januari 7,2024.


Vile vile amempongeza mbunge wa jimbo la Nkenge Frolent Kyombo kwa kuwapa ushirikiano Wananchi Wilayani Misenyi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha katika miradi ya maendeleo huku akimuomba mbunge huyo kuwatengenezea barabara na kumuwezesha kujenga kituo cha kukusanyia maziwa Bubale.


Alitumia fursa hiyo kuwataka Wananchi walioko Jimbo la Nkenge kujiunga na mradi huo kupitia ushirika wa Bubale na ushirika wa maziwa Nsunga.

Post a Comment

0 Comments