Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) wametakiwa kuimarisha utalii wa misitu Ikolojia kwa kuvilinda na kuviendeleza vivutio hivyo ili kuendelea kuvutia watalii wa ndani na wa kimataifa ili kufikia mpango wa taifa wa kufikisha idadi ya watalii wapatao milioni 5 na mapato ya Taifa dola bilioni 6 ifikapo 2025.
Rai hiyo imetolewa jijini Arusha na Naibu katibu Mkuu(Utalii),wizara ya maliasili na utalii ,Mkoba Mabula wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wahifadhi wa TFS wanaosimamia utalii katika hifadhi za misitu na vituo vya mali kale kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Alisisitiza kuwa mafunzo hayo yalenge kuendeleza mazao ya utalii, ukarimu na masoko,matumizi ya mifumo ya tehama ,usimamizi wa mitandao ya kijamii na uandaaji wa maudhui.
Alisema sekta ya utalii imeendelea kuwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa kwa kutoa fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa sekta zingine kiuchumi.
"Sekta ya utalii imeendelea kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 17.2 kutokana na fedha za kigeni,huku wageni wakiongezeka kwa mwaka 2023 watalii walifikia zaidi ya milioni 1.8 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019 kabla ya janga la Covid 19 sawa na ongezeko la asilimia 18".
Kadhalika alisema mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kwa asilimia 31 hadi kufikia dola za kimarekani bilioni 3.4 mwaka 2023,kutoka Dola bilioni 2.6 mwaka 2019.
Alisema mafanikio hayo yametokana na kuvitangaza vivutio vya utalii kwa ubora ikichagizwa na maeneo mahususi kama mbunga za wanyama kama Serengeti ,mlima Kilimanjaro,Bonde la Ngorongoro ,fukwe na maeneo mengi ya historia ya Mali kale pamoja na misitu ya Ikolojia mbalimbali.
Alisisitiza lazima maeneo hayo yalindwe na kuendelezwa ili kuyafikia masoko ya kimkakati na kuwavutia watalii wengi na wawekezaji.
Awali Kamishna wa Uhifadhi Prof Dos Santos Silayo alisema TFS imejiwekea mkakati wa kukuza uhifadhi wa misitu hapa nchini ikiwemo kupandisha hadhi ya maeneo ya misitu na kufikia 25.
Akiongelea manufaa yaliyopatikana kwa mwaka 2019 kabla ya covid 19 ,alisema waliweza kupata watalii wapatao 57,000 na kuwezesha kupatikana kwa mapato ya sh,bilioni 150 .
"Leo tukizungumzia utalii katika maeneo ya misitu tunapata wageni 250,000 na mapato ya sh, bilioni 1.9 kwa mwaka, na mwaka huu wa fedha 2024/25 lengo letu ni kufikisha wageni 300,000 na mapato yasiopungua sh, billion 3."alisema.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utalii Dkt Thereza Mngobi aliwapongeza TFS kwa kazi nzuri ya kusimamia sera na sheria za utalii na kanuni zake.
Ends..
0 Comments