TAZAMA PICHA 10 WAGONJWA WAKIPATIWA HUDUMA ZA MATIBABU YA KIBINGWA BURE NA MADAKTARI BINGWA HOSPITALI YA RUFAA MOUNT MERU ARUSHA.

Na Joseph Ngilisho,ARUSHA

 

Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha ,Mount Meru imejipambanua kutoa huduma za matibabu ya kibingwa bure kwa wagonjwa takribani 4000 katika kipindi cha siku tatu ikiwa ni mpango wake wa kusaidia watu wenye changamoto ya afya katika kuadhimisha sherehe za miaka 63 ya Uhuru.


Akiongea katika viwanja vya hospitali hiyo wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo mapema leo Desemba 6, 2024 Daktari Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Alex Ernest alisema mwitikio umekuwa ni mkubwa na katika siku ya uzinduzi watu zaidi ya 500 wameonwa na kupatiwa matibabu na madaktari bingwa  wa hospitali hiyo .


Aliwataka  wakazi wa Arusha  kujitokeza kwa wingi katika hospitali hiyo ili kunufaika na fursa hiyo  ya kupata matibabu yanayotolewa bure.



Alisema katika kampeni hiyo, zaidi ya madaktari bingwa 30 watakuwepo ambapo hadi kukamilika kwa zoezi hilo Disemba 9, 2024 wanatarajia jumla ya wakazi 4000 wa jiji la Arusha wataweza kupata tiba za kibingwa ikiwa ni wastani wa wagonjwa 1000 watakuwa wakitibiwa kwa siku.


“Tunawatangazia wakazi wote wa Arusha wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali wafike hospitalini hapa kwaajli ya kupata tiba ya bure, wataweza kuwaona madaktari bingwa na kuhudumiwa kwa uangalizi wa hali ya juu,”amesema.


Amesema wagonjwa watakaolazimika kufanyanyiwa upasuaji, watalazwa na kupewa huduma hiyo bure katika hospitali hiyo lakini watakaolazimika kupewa rufaa hao watajigharamia huko watakapohamishiwa kwa kuwa huduma za bure ni katika hospitali hiyo pekee.


Dkt Ernest amesema zaidi ya huduma 15 zitatolewa kupitia madaktari bingwa hao ikiwemo huduma za mama na mtoto, magonjwa ya mfumo wa mkojo, kinywa ikiwemo pua na masikio, meno, macho, ngozi, kisukari, huduma za mifupa, pathologia, magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, shiniko la damu n.k.


Amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ni changamoto kubwa nchini kwa kuwa waathirika wamekuwa wakigundua kuwa nayo wakati ugonjwa ukiwa umeshasambaa kwa kiasi kikubwa kutokana na kutokuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara.


“Kupitia kampeni hii pia tutakuwa tukitoa elimu kwa wagonjwa kuhusiana na mfumo wa maisha ili kuweza kubadili mfumo wao wa maisha wanaoishi ambao ndio umekuwa ukisababisha magonjwa mengi yasiyoambukiza,”amesema.


Dkt Ernest amesema pia kampeni hiyo imeletwa ili kutaka wananchi kujionea namna serikali ilivyowekeza kwenye sekta ya afya nchini kwa kufanya mapinduzi makubwa ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara.


“Lakini lengo lingine ni kutaka kufikia wananchi wale wasiokuwa na uwezo wa kupata huduma za kibingwa kutokana na changamoto nyingi ikiwemo gharama zake kuwa kubwa kuweza kuzipata, pia kusogea karibu huduma kwa wananchi,”amesema.












Ends...



Post a Comment

0 Comments