RC Mwassa atoa matokeo ya mwanzo tamasha la Ijuka Omuka awapa kongole wana Kagera
Na Lydia Lugakila
Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa amewashukuru na kuwapongeza Wananchi na Viongozi wa dini Mkoani humo kutokana na kushiriki ipasavyo katika tamasha la Ijuka Omuka linalolenga kuwakumbusha wazawa wa Mkoa huo waishio nje na ndani ya Nchi kukumbuka na kurudi kuwekeza nyumbani.
Akizungumza na vyombo vya habari Desemba 22, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajjat Fatma Mwassa alisema kuwa Tamasha hilo linaloendelea Mkoani humo tayari limezaa matunda makubwa kwa muda mfupi hadi sasa.
Mwassa ametaja mafanikio ya muda mfupi yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kuwakutanisha wanakagera kujadili masuala mbali mbali yanayohusu Mkoa huo, kubwa likiwa ni kujadili maendeleo yaliyolenga kuufufua upya Mkoa huo na kutangaza fursa zilizopo ambazo zimeeleweka kwa haraka ikiwa ni pamoja na Desemba 21 mwaka huu kumpokea Bilionea mwekezaji aitwaye Mulokozi ambaye amefika na kueleza nia yake ya kufanya uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha Kahawa mwaka 2025.
Aidha aliwapongeza Wananchi wa Mkoa huo kwa kujitokeza kwa wingi katika tamasha la Ijuka Omuka ambapo pia Aliwashukuru Viongozi wa dini kwa kuonyesha ushirikiano mzuri katika maombezi ya kuliombea Taifa, Mkoa na kumuombea Rais Samia pamoja na wasaidizi wake ambapo
"Nipongeze juhudi hizi za Ijuka Omuka tumepata mwekezaji Mulokozi tutampa ushirikiano wa kutosha na kupitia wenzake kitajengwa pia kiwanda cha nyama, kiwanda cha madawa ya binadamu Mkoani hapa yote haya ni matokeo ya Ijuka omuka " alisema Mwassa.
Amemkaribisha mwekezaji huyo na kumuahidi kumkabidhi eneo la kujenga kiwanda cha Kahawa ndani ya siku 14.
RC Mwassa amewaomba wanakagera wengine wenye uwezo na wenye mtaji kumuunga mkono ili kuiendeleza Kagera.
Kupitia tamasha hilo yapo maonyesho mbali mbali yanayoendelea katika viwanja vya CCM Bukoba lengo likiwa ni kuongeza mtandao wa biashara ambapo Mkuu huyo wa Mkoa ametumia fursa hiyo kuwaomba wajasilia mali, waendesha pikipiki, wamiliki wa hoteli, Mama lishe kuchangamkia fursa mbali mbali zinazotokana na tamasha hilo.
Aliongeza kuwa tamasha hilo limeleta umaarufu mkubwa kwani kupitia utamaduni wanakagera wamecheza ngoma ya asili,wamekula chakula cha asili kwa mtindo wa kiasili na wameshuhudia mziki wa kizazi kipya.
Hata hivyo Mwassa amewashukuru Viongozi wa dini waliotumia muda wao kufanya maombezi huku akiwapongeza machifu kwa kuonyesha kuenzi mila, tamaduni na desturi za Mkoa huo huku akiwaomba kuendelea kujipatia bidhaa zinazouzwa katika maonyesho hayo yanayoendelea hadi Desemba 26,2024.
0 Comments