By Ngilisho Tv-ARUSHA
Mtandao wa Jeshi la Polisi Wanawake Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na dawati la Jinsia na watoto katika kuelekea kilele cha siku 16 za kupinga ukatili, leo wametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu wanawake walioko katika gereza Kuu Arusha.
Akikabidhi msaada huo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Georgina Matagi kwa niaba ya Mwenyekiti wa Mtandao huo, amebainisha kuwa Jeshi la Polisi linashirikiana na makundi yote katika jamii kupinga na kukemea vitendo vya ukatili.
SSP Matagi ameendelea kufafanua kuwa waliona ni vyema mwaka huu katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili kwenda kuwatembelea wafungwa gerezani kwa ajili ya kuwapa moyo na hamasa ili pindi wanapomaliza vifungo vyao kuwa mabalozi wazuri wa kupinga na kukemea vitendo hivyo katika jamii.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Gereza Kuu Arusha Kamishna Msaidizi wa Magereza ACP Charles Mihinga amelishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada huo na kuahidi kila kilicholetwa kitatumika kama ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa jamii kuwa na moyo wa kusaidia wahitaji hususani waliopo gerezani.
Naye Daktari wa Gereza hilo Mkaguzi wa Magereza INSP Christine Buhinu amesema kitendo cha Jeshi la Polisi kwenda kuwatembelea wafungwa na kuwapa misaada, kitawapa moyo wafungwa hao lakini pia kuona jamii inawakumbuka na haijawatenga.
Kwa upande wake Konstebo wa Polisi Latifa Juma ametoa wito kwa askari wenzake kuendelea kuyakumbuka makundi yenye uhitaji katika jamii kwa kuyapatia misaada lakini pia kutoa elimu juu ya kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Misaada iliyotolewa ni pamoja na magodoro, sukari, Televisheni, King’amuzi na mahitaji mengine ya muhimu ambayo walikua na uhitaji nayo
0 Comments