By Ngilisho Tv KILIMANJARO
WATU sita wamefariki dunia huku nyumba 25 zikibomoka sambamba na uharibifu wa mazao na miundombinu ya barabara wilayani Same, mkoani Kilimanjaro kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Same, Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni, aliwaambia waandishi wa habari wilayani humo jana kuwa hadi kufikia asubuhi ya jana, mvua hiyo imeleta madhara hayo.
Alisema miundombinu ikiwamo ya barabara hasa zinazoelekea kata za milimani imeharibiwa na kufanya baadhi ya maeneo kutofikika kwa urahisi.
Alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa ndugu na jamaa walioathiriwa na majanga hayo yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha wilayani humo.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya maafa ya wilaya hiyo, maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na kata za Msindo, Vuje, Bombo, Mtii na Maore ambako serikali inaendelea kufanya tathmini kupitia kamati ya maafa wilaya ili kujua ukubwa wa athari za mafuriko hayo na taarifa zake zipelekwe ofisi ya mkoa kwa ajili ya kufikishwa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu kwa hatua zaidi.
Mkuu wa Wilaya huyo aliwataka wananchi kuendelea kuwa na tahadhari ikiwamo kuhama kwa muda katika maeneo hatarishi ili kuepusha madhara zaidi ya kibinadamu na mazingira.
Mgeni akawaasa wananchi walio katika maeneo yaliyokumbwa na maafa kuwa watulivu wakati huu ambao serikali inaendelea na tathmini ya athari ya mafuriko.
"Mipango mbalimbali inaendelea kufanywa ili kuhakikisha miundombinu yote iliyoharibiwa na mvua inarejeshwa katika hali yake," alisema Mkuu wa Wilaya.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kilimanjaro, Mkaguzi Msaidizi Jeremiah Mkomagi aliwataja waliofariki dunia ni Joyce Elifuraha (57) na mumewe Elifuraha Elienea (59), wakazi wa kijiji cha Mjema.
Wengine ni Hamu Ally (76), mkazi wa kijiji cha Miombo, Kata ya Mtii; Elibariki Fanuel (48), mkazi wa kijiji cha Vuje, Lazaro Saikon (35), mkazi wa kijiji cha Mheza na Eliakunda Elisafi (69), mkazi wa kijiji cha Duma.
Alisema: "Kuanzia Desemba 20 hadi 22 tumepokea taarifa za vifo vya watu sita katika wilaya ya Same na majeruhi wanne, wanaume wawili na wanawake wawili ambao wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Gonja Lutheran na hali zao zinaendelea vizuri."
0 Comments