Na. Coletha Charles, DODOMA
Madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Makete na Igunga wametakiwa kushirikiana na wananchi katika shughuli za kila siku ili kuweza kukuza uchumi na maendeleo ya halmashauri zao.
Rai hiyo litolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe wakati akiwakaribisha madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete na Igunga waliotembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kujifunza shughuli mbalimbali za uendeshaji wa halmashauri pamoja na kuanzishwa miradi mikubwa ya maendeleo. “Halmashauri zetu zihakikishe zinabuni vyanzo vingine vya mapato, pamoja na kuboresha ile iliyopo ili serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iweze kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi. Lakini iwe rai yetu wote tujipime kabla hatujapimwa” alisema Prof. Mwamfupe.
Sambamba na hilo, aliwapongeza madiwani hao kwa kushirikiana vizuri katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Nae, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga, Swela Hamid alimshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwapokea na kuwapa ujuzi na elimu ya namna ya kutekeleza miundombinu na uwekezaji katika wilaya yao. “Tumeona kikubwa siyo fedha. Wenzetu wana fedha zao ziko zaidi ya shilingi bilioni 60 na sehemu kwa mapato ya ndani, sisi fedha zetu mapato ya ndani ni shilingi bilioni tano. Lakini kikubwa nilichojifunza leo ni udhubutu na kuanzisha miradi ambayo halmashauri inaweza ikaendesha yenyewe bila kuitegemea serikali na ushirikiano kwa pamoja tunaweza kuinua halmashauri yetu kiuchumi” alisema Hamid.
Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda alisema kuwa ziara ya kuitembelea Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatija kwa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, ili wakafanye maamuzi sahihi ya kuhakikisha maendeleo yanakua kwa kasi na wananchi wananufaika na ukuaji wa uchumi.
Ikumbukwe kuwa madiwani wa Halmashauri za Wilaya ya Makete na Igunga, wameongozwa na wenyeviti wa halmashauri hizo, wakuu wa Divisheni na Vitengo katika ziara ya mafunzo ili kuweza kujionea namna bora ya kuendesha miradi ya maendeleo.
Ends....
MWISHO
0 Comments