Makampuni ya Ulinzi Arusha yakumbushwa kuzingatia sheria za ukamataji Salama.
Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeendelea kutoa elimu na mafunzo kwa askari na wamiliki wa makampuni binafsi ya ulinzi lengo likiwa ni kuwajengea uwezo askari hao juu ya ukamataji salama,vitendo vya ukatili pamoja na kufahamu dhana ya Polisi Jamii.
Akihitimisha mafunzo hayo leo Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Arusha Mrakibu wa Polisi SP Happiness Temu amewataka wamiliki na askari wa makampuni hayo ya ulinzi kuzingatia sheria walizofundishwa na zilizopo katika vitabu vya sheria ili kutekeleza majukumu yao kwa weledi Mkubwa.
SP Temu ameongeza kuwa makampuni hayo yanayo nafasi pia katika kutokomeza ukatili mahala pa kazi na jamii kwa ujumla huku akiwaomba kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutomeza vitendo vya ukatili
Sambamba na hilo amewaomba kuendelea kufichua uhalifu na wahalifu ili Mkoa wa Arusha uendelee kuwa na sifa nzuri ya kupinga vitendo vyote vya uhalifu,kitendo ambacho kitachochea na kushawishi wageni wa ndani na nje ya nchi kutembelea Mkoa wa Arusha ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini.
0 Comments