RAIS MWINYI: UWANJA WA NDEGE ZANZIBAR KUWA NA HADHI YA KIMATAIFA.
By Ngilisho Tv-Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uimarishaji wa miundombinu katika Uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kunalenga kuvifanya kuwa bora na kutoa huduma kulingana na vigezo vya Kimataifa.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 21 Disemba 2024 alipozindua miradi miwili na kuweka mawe ya msingi katika miradi mitatu ya miundombinu mbalimbali katika kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, Wilaya ya Magharibi B, ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha Rais Dk. Mwinyi ameeleza kuwa lengo ni kuwa na Viwanja vya ndege vyenye sifa ya utoaji wa huduma bora kwa abiria zitazokidhi mahitaji ya ongezeko la wageni wanaoingia nchini kila siku.
Amefahamisha kuwa miradi aliyoizindua itaufanya uwanja huo kuwa wa kujivunia na hadhi ya Kimataifa katika Afrika na duniani kwa utoaji wa huduma bora zitakazoridhiwa na wageni.
Miradi aliyoizindua Dk. Mwinyi ni pamoja Uwekaji wa mawe ya msingi kwa majengo ya abiria “Terminal 1 na 2, ambayo ameielezea itajumuisha ujenzi wa jengo la viongozi na wageni mashuhuri (VIP) utakaotumiwa pia na wafanyabiashara wakubwa, kupokea ndege binafsi za wageni mashuri.
Akizungumzia ukuaji wa utalii nchini amesema takriban watalii milioni mbili wanaingia nchini kila mwaka, hivyo kuna kila sababu kwa Serikali kuchukua juhudi maalum za kuimarisha viwanja vya ndege kwa miundombinu bora.
Vilevile Rais Dk. Mwinyi ameahidi ujenzi wa hoteli kubwa zenye hadhi ya juu ili kuwavutia wageni wengi zaidi hatua itakayoimarisha utalii na kuongeza mapato yanayotokana na sekta hiyo muhimu kiuchumi.
0 Comments