By Ngilisho Tv-Dar Es Salaam
WANAODAIWA kuwa wamiliki wa jengo la ghorofa Kariakoo ambalo liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 31, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma za kuua bila kukusudia.
Washtakiwa waliofikishwa mahakamani hapo ni Leon Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61) mkazi wa Kariakoo na Ashour Ashour (38) mkazi wa Ilala na wote ni wafanyabiashara.
Wakisoma hati ya mashtaka jopo la mawakili watatu wa serikali , Adolf Lema, Grace Mwanga na Eric Kamala mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Godfrey Mhini, ilidaiwa kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa mashtaka 31.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao, Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, Kariakoo jijini Dar es Salaam, isivyo halali, kwa pamoja walishindwa kutimiza majukumu na kusababisha vifo vya watu 31.
Watu hao waliofariki ni Said Juma, Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Chatherine Mbilinyi.
Wengine ni Elton Ndyamkama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuf, Ally Omary, Ajuae Iyambilo, Mary Lema, Khatolo Juma, Sabas Swai, Pascal Ndungulu, Brigette Mbembele, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Issa Bakari, Lulu Sanga, Happnees Mallya na Brown Kabovera.
Baada ya kuwasomea mashtaka hayo, Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao, hivyo hawatakiwi kujibu chochote.
Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Mhini alisema ili washtakiwa wawe nje kwa dhamana, wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wenye barua za utambulisho, kitambulisho cha taifa na watatakiwa kutia saini bondi ya Sh. milioni tano kila mmoja.
Mshtakiwa Mdete alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana lakini Islam na Ashour walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti hayo.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 12, mwaka huu, kwa kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia
0 Comments