Na Joseph Ngilisho ARUSHA
WASHIRIKI wa kozi ndefu kutoka Mataifa 16 ikiwemo Tanzania kutoka chuo cha ulinzi cha taifa,(NDC) ,wamefanya ziara ya kimasomo mkoani Arusha kwa lengo la kujifunza kwa vitendo ili waweze kuwa kitovu cha kuwezesha maamuzi ya Serikali kwenye kila sekta yanayozingatia tija na usalama wa taifa.
Akizungumzia umuhimu wa ziara hiyo leo Novemba 11,2024 kwa kundi la 13 la kozi ndefu ya wiki 47 ya mafunzo ya usalama wa kimkakati ,Mkuu wa chuo hicho Meja Jenerali Wilbert Augustine Ibuge alisema ujumbe huo unahusisha viongozi wa ngazi za juu na maafisa waandamizi kutoka Vyombo vya ulinzi, Wizara, Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali ambao baada ya mafunzo hayo watakuwa ni washauri wazuri wa Serikali na wafanya maamuzi wa kimkakati.
“Tupo kwenye kipindi cha mafunzi ya Uchumi na Utalii ikiwa ni sehemu ya moduli tulizonazo na ziara hii tunaifanya kila mwaka kwasababu tunajua mchango wa Mkoa wa Arusha kwenye Sekta ya utalii na Uchumi kwa Ujumla ni mkubwa sana kwenye Taifa letu”. Amesema.
Hata hivyo washiriki wa kozi hiyo iliyoanza Septemba Mwaka huu ni 61 huku washiriki 40 wakiwa ni Watanzania na wengine 21 kutoka nchi 16 ikiwemo india, Misri na Ephiopia.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Rashid Mkombachepa amewakaribisha wajumbe hao na kusema kuwa ziara hiyo ni muhimu hasa kwa kuendeleza jitihada za kukuza sekta ya Utalii hasa kwa mkoa wa Arusha amba oni kitovu cha Utalii.
“Nimefurahi sana kujumuika kwenye ziara hii Mkoani hapa na kujifunza mambo mengi kuhusu Utalii ikiwa ni sehemu ya mafunzo yetu, Nchi ya Tanzania na India zimekuwa na ushrikinao mzuri kihistoria tangu niliposikia Azimio la Arusha chini ya Baba wa Taifa Mwl. Nyerere”.Alisema mmoja ya washiriki hao kutoka Jeshi la India, Group Captain Nitesh Chauhan.
Wajumbe hao watakuwa mkoani Arusha kwa muda wa siku nne na kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii.
Naye mshiriki wa kozi hiyo ya ulinzi wa Taifa, Brigedia General Hasan Mabena alisema ziara hiyo imelenga kujifunza masuala ya sekta ya utalii nchini kwa lengo la kutangaza na kukuza utalii kwa maendeleo ya kijamii na uchumi wa Tanzania.
Ends..
0 Comments