Na Joseph Ngilisho ARUSHA
HAKIMU Mfawidhi wa Mahakama ya hakimu Mkazi Arusha, Erasto Philly amesisitiza upande wa Mashtaka kuhakikisha upelelezi unakamilika kwa wakati katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mwekezaji na Mfanyabiashara Saleh Salim Alamry(54) na wakili wa kujitegemea Shecky Mfinanga na kutamka ya kwamba mahakama isitumike kama ngazi ya kuwatesa watuhumiwa.
Hata hivyo upande wa mashtaka umeieleza mahakama hiyo kwamba upelelezi wa shauri hilo upo mbioni kukamilika na ndani ya wiki moja watakamilisha .
Mwekezaji Saleh anashikiliwa katika mahabusu ya gereza Kuu la Arusha,Kisongo, kwa zaidi ya siku 80 tangu alipokamatwa agosti 22 mwaka huu,akikabiliwa na makosa 27 yakiwemo ya uhujumu uchumi ,utakatishaji wa fedha na kuongoza genge la uhalifu na kusababisha hasara ya dola milioni 26 ,hata hivyo mshtakiwa mwenzake Mfinanga yupo nje kwa dhamana.
Hatua hiyo imekuja kufuatia wakili wa serikali Mahfudh Mbagwa kudai mbele ya mahakama ya hakimu Mkazi Arusha kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na kuahidi kukamilisha ndani ya wiki moja ijayo kuanzia leo Novemba 7,2024.
Wakili Mbagwa aliiambia mahakama hiyo kwamba baada ya wiki moja upelelezi utakuwa umekamilika, "tunaomba tarehe nyingine ya kutajwa wakati jitihada za kukamilisha upelelezi zinaendelea".
Awali jopo la mawakili wa upande wa utetezi wakiongozwa na wakili Faisal Rukaka na wenzake Moses Mahuna, Denis Mworia na Kerry Mra ,wakili Rukaka alisema
"Tumesikia upande wa Jamhuri wakisema upelelezi bado ila wanatarajia wiki ijayo wawe wamekamilisha , Pia katika muktadha huo tunaomba ofisi ya DPP itoe consent kwa Mahakama hii(hati au ruhusa au mamlaka) ili isikilize kesi hii na kutoa baadhi ya amri"
"Pia tunaomba suala hili la upelelezi lifanyike kwa haraka kwa sababu kosa la mteja wetu halina dhamana anakosa kufanya shughuli zake za kila siku." aliieleza Mahakama
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Erasto Philly aliwajia juu upande wa mashtaka akidai kwamba mahakama isitumike kama ngazi ya kutesa watuhumiwa na kuitaka jamhuri ikamilishe upelelezi haraka.
"Wasipokamilisha upelelezi haraka watakuwa wanaitumia mahakama kama ngazi ya kumtesa mtuhumiwa ,upande wa mashtaka hakikisheni upelelezi unakamilika haraka sio kila siku kuja kusema upelelezi haujakamilika".
"Kuna nafuu tatu ambazo mnaweza kuzitumia ambazo ni kuipa mahakama hii mamlaka ya kusikiliza shauri hili, kulipeleka Mahakama Kuu au kuwaachia huru watuhumiwa (NOLLE PROSEQUI). Ni vema waendesha mashitaka mkafanya mawasiliano na wapelelezi kuliko kuja kuwasemea wao hapa"alionya hakimu
Baada ya maelezo hayo hakimu Philly aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 21 Mwaka huu itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa
Ends..
0 Comments