Na Joseph Ngilisho ARUSHA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania [TIRA] Mkoa wa Arusha imeanzisha mpango wa kuwapatia elimu ya umuhimu wa kujiunga na huduma za bima sanjari na kuanzisha vilabu kwa zaidi ya walimu 50 wa shule ya msingi na Sekondari katika halmashauri ya Arusha (Arusha DC) wilayani Arumeru Mkoani Arusha.
Akiongea na vyombo vya habari katika mafunzo hayo yaliyofanyika katika shule ya Sekondari Mringa,wilayani humo,Meneja wa TIRA kanda ya Kaskazini, Bahati Ogola alisema mafunzo hayo yamelenga kuwapatia elimu ya Bima walimu ili kuwa mabalozi wazuri wa kufundisha wanafunzi na jamii kwa ujumla umuhimu wa kuijua na Bima na manufaa yake.
"Kupitia Mabalozi hao naimani elimu watakayoipata watakwenda kuhamasisha kuanzisha vilabu vya bima ili jamii pamoja na wanafunzi wajue umuhimu wa kujiunga na bima na faida zake"
Alisema wamechagua kundi la walimu kuwa mabalozi wa bima kwa kuwa wanaamini walimu ni kundi muhimu kwa jamii na wanauzoefu wa kuenez elimu hiyo kupitia vilabu watakavyoviunda mashuleni ili kuwajenga wanafunzi kuijua Bima wakiwa na umri Mdogo.
Walimu wanaopata mafunzo haya ni wawakilishi kutoka shule 60 zilizopo katika halmashauri hiyo na kwamba zoezi la kuanzisha vilabu mashuleni kupitia walimu ni endelevu na kila shule itakuwa na Klabu yake.
Ogola aliitaka jamii kuchangamkia fursa za Bima ili kuweze kunufaika na huduma za Bima katika kurahisisha shughuli zao za kiuchumi na maendeleo .
Baadhi ya walimu waliopatiwa mafunzo hayo ,Mwalimu Evance Katunzi wa shule ya sekondari Mringa,ameyapongeza mafunzo hayo ambayo yamemfumbua macho kujua umuhimu wa Bima katika kusaodia majanga ya kibinadamu yanapotokea.
Alisema Elimu hiyo ataifikisha kwa jamii hususani wanafunzi ili kuwahamasisha umuhimu wa kujiunga na bima na kujua faida zake.
Naye mwalimu Upendo Mwakasata kutoka shule ya sekondari Kiserian alisema amenufaika sana na elimu ya Bima kwa kuwa hapo hawali hakuona umuhimu wa kujiunga na Bima na kwamba jamii bado haina mwamko wa Bima kutokana na uoga na amejipanga elimu hiyo kuwanufaisha na wengine baada ya kuwa balozi mzuri.
"Mimi leo nimenufaika sana na elimu ya Bima na nimeona upo umuhimu wa kujiunga na Bima kwani unaweza kuwekeza kwenye bima ya maisha pia naweza kuwekea bima hata kwenye Nyumba yangu kujikinga na majanga ya kibinadamu"
Ends...
0 Comments