By Ngilisho Tv Dodoma
MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini M.Sedoyeka, leo Oktoba 16,2024 amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili kwa malalamiko Manne ya kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
Malalamiko hayo ni kumpandisha cheo mtumishi kwa upendeleo, kuingilia mchakato wa ununuzi wa viti na meza, kuwa na uhusiano wa karibu na mtumishi na kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi kinyume na maadili ya viongozi wa umma.
Kikao cha baraza hilo kimeketi leo jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Baraza Jaji Mstaafu Rose Teemba na upande wa mlalamikaji umewakilishwa na Mawakili wa Serikali Bi.Emma Mwite na Hassan Mayunga.
Akisoma hati ya malalamiko mbele ya Baraza,Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Emma amesema kuwa Prof. Sedoyeka akiwa anatekeleza majukumu yake ya uongozi pasipo kufuata Sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma alimpandisha cheo Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimali II kuwa Mkuu wa Sehemu ya Rasilimaliwatu kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi huyo na bila kuwa na sifa na vigezo.
Pia, amesema malalamiko mengine kuwa na uhusiano wa ukaribu na Hakim Datama kwa kufanya naye kazi IAA na kisha Wizara ya Maliasili na Utalii na aliporudishwa tena IAA, Mtumishi huyo aliombewa ahamie IAA mara tu baada ya mlalamikiwa kuteuliwa kuongoza taasisi hiyo.
“Jambo jingine linalolalamikiwa ni kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza katika Kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na bila sababu za kisheria,” amesema.
Pia, Prof.Sedoyeka anakabiliwa na malalamiko ya kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi Robert Mwintango (Afisa Ugavi) kutoka Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kwenda Idara ya Maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi.
Akitoa ushahidi mbele ya Baraza hilo Afisa wa Sekretarieti ya maadili kwa viongozi wa Umma Dodoma Malalamikiwa Ramadhan Mwanang’waka amesema katika uchunguzi wao walibaini kuwa malalamikiwa alifanya uteuzi wa mtumishi Hakimu Datama kuwa mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu kinyume na sheria na taratibu kwasababu mtumishi huyo aliteuliwa katika wadhifa huo wakati alikuwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na alikuwa akifanya kazi kwa kuazimwa katika chuo hicho.
Shahudi huyo amesema kingine walichokibaini ni kuwepo kwa mgongano wa mslahi kwa Mkuu huyo katika majukumu yake ikiwemo suala la upendeleo kwa mtumishi huyo kwa kumteua katika nafasi ya uongozi hali kuwa ni mtumishi ambaye alikuwa ni Afisa daraja II na hakuwa nasifa za kuteuliwa kuwa mkuu wa Taasisi katika utumishi wa umma.
Kulingana na Maelezo ya mlalamikiwa alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa alikuwa akimuamini, licha ya kuwa wakati anateuliwa mtu huyo kwenye kitengo hicho alikuwepo afisa mwingine ambaye alikuwa na sifa za kuteuliwa kuwa mkuu wa idara tofauti na yule aliyeteuliwa ambaye Prof. Sedoyeka anadai alimsomesha mtu huyo mpaka kumuamini na kumpatia cheo ila baada ya kuulizwa kwanini kafanya hivyo alisema hakuwa na umahili wa nafasi hiyo.
Shauri hilo litaendelea kesho ambapo mashahidi wengine wawili watatoa ushahidi wao majira ya saa 3 asubuhi.
Ends..
0 Comments