Na Joseph Ngilisho ARUSHA
MWEKEZAJI na mfanyabiashara katika sekta ya uwindaji wa kitalii na Kilimo nchini, Saleh Salim Alamry(54) mkazi wa Njiro jijini Arusha, ameendelea kusota katika mahabusu ya gereza kuu la Arusha,Kisongo , kwa kile kinachodaiwa ni shinikizo kutoka kwa Wabia wenzake ambao wanapata nguvu kutoka kwa mtoto wa kigogo wa ngazi za juu na ameiomba serikali kuingilia kati ili haki iweze kutendeka.
Saleh ambaye ni mbia wa kampuni ya Sunset Tarangire limited na Alrajhi Holdings LTD,alikamatwa Agosti 22,mwaka huu 2024 na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU mkoa wa Arusha baada ya kupokea wito kutoa kwa mmoja ya maofisa wa taasisi hiyo.
Hata hivyo akiwa chini ya ulinzi wa Takukuru Arusha , Saleh alihoji sababu za yeye kushikiliwa na Taasisi hiyo lakini aliambiwa ni maelekezo kutoka ngazi za juu na makosa yake atayajua siku akifikishwa mahakamani na kama anamalalaiko aandike barua.
Mwekezaji huyo ambaye anatetewa na Wakili Moses Mahuna akishirikiana na Wakili Faisal Rukaka ambao tangu awali wamekuwa wakisimamia mgogoro wa mwekezaji huyo na wabia wenzake. Hata hivyo, Wakili Faisal alisema kuwa mteja wao alifikishwa mahakamani Agosti 28 mwaka huu na kusomewa mashtaka 27 yakiwemo ya uhujumu uchumi , utakatishaji wa fedha na kuongoza genge la uhalifu ambayo kisheria hayana dhamana.
Pia anadaiwa kufanya udanganyifu kwa kughushi nyaraka mbalimbali za umiliki wa kampuni ya Sunset Tarangire limited kwa kutengeneza hati za uongo kinyume na makubaliano na washirika wenzake Khaled Alrajhi na Abdulkarim Alrajhi wanaoishi nchini Saud Arabia.
Mariam Salumu ambaye ni ndugu wa mshtakiwa amemwomba Jaji Mkuu kuingilia kati ili kusaidia ndugu yake kuoata haki yake ya msingi kwani wabia wenzake wanatumia vibaya mahakama kumgandamiza ili apoteze hisa zake alizowekeza kwa muda mrefu.
Mahakama imekuwa ikidai haijapewa kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP ambaye huwakilishwa na Wakili wa serikali Edgar Bantulaki.
"Kwa mara ya tatu mfululizo shauri hilo limeitwa mahakamani na mahakama kudai haijapewa kibali cha kusikikiza huku ndugu yetu akiendelea kusota magereza tunahisi kuna mchezo mchafu wenye nia ovu ya kupindisha haki ya msingi ya ndugu yetu akose haki yake na tunamwomba jaji Mkuu aingilie kati ili mshtakiwa ajue haki zake"Alisema Mariamu
Hata hivyo taarifa kutoka katika chanzo cha kuaminika zinasema kuwa Wawekezaji wenzake wamediriki kutamka kwamba "Endapo mtu yeyote atafanikiwa kumtoa Saleh rumande basi wao watampa kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni Kumi , jambo ambalo ndugu zake wameiomba serikali kuingilia kati ili haki itendeke.
Septemba 12 mwaka huu,Saleh alifikishwa mahakamani ambapo wakili wake ,Moses Mahuna aliiomba mahakama iwasisitize upande wa Jamhuri kuleta kibali ama consent au imwachie huru mtuhumiwa ili pale itakapokamilisha upelelezi mshtakiwa akamatwe, Wakili wa serikali Edgar Bantulaki aliieleza mahakama kuwa upelelezi hauja kamilika na utakapo kamilika hawajui endapo wataendelea na mashtaka haya wanayomshikilia nayo au la!
"Hivyo ni ngumu kuleta kibali cha DPP kuridhia uendeshwaji wa kesi katika mahakama hiyo ya hakimu mkazi kwa kuwa mpaka sasa hawajui watamshitaki mtuhumiwa na makosa gani" Wakili Edgar aliiambia mahakama
Mwingine anayeshtakiwa katika shauri hilo namba 24767/2024 ni Wakili wa kujitegemea Sheck Mfinanga ambaye anashtakiwa kwa makosa sita ,ambayo ni pamoja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kuongoza genge la uhalifu na kughushi na yupo nje kwa dhamana baada ya mashtaka yake kuwa na dhamana ya kisheria.
Wakiongea na waandishi wa habari nje ya mahakama, wakili wa utetezi, Moses Mahuna na Faisal Rukaka walisema kuwa June 14,2024 kampuni hizo zilifungua kesi ya madai katika mahakama ya biashara jijini dar es salaam zikidai mwekezaji mwenzao(Mshtakiwa)ambaye anahisa 51 katika uwekezaji wa kampuni hizo hakuwa mwaminifu na hakuzingatia makubaliano ya uwekezaji na kusababisha hasara ya dola za kimarekani milioni 26.
Wakati shauri hilo likiendelea Julai mwaka huu Saleh aligundua kuwa wawekezaji wenzake wameghushi saini yake na kujipatia mamlaka ya kikampuni ya kumfuta nafasi ya ukurugenzi pasipo yeye kuhusika.
Wakili Faisal Rukaka aliongeza na kusema kuwa mteja wao alilazimika kutoa taarifa kituo kikuu cha polisi Arusha na shauri hilo lilifunguliwa na baadaye kutua ofisi ya mkuu wa upelelezi Mkoa RCO.Hata hivyo hakuna hatua zozote zilizochukuliwa ikiwemo kuwahoji watuhumiwa, ndipo alipoamua kuandika barua ya malalamiko ngazi za juu za polisi kulalamikia kutoitwa wala kuhojiwa kwa watuhumiwa wake(wakurugenzi Wenza)
"Baada ya malalamiko yake kufika ngazi za juu za polisi jalada la kesi hiyo liliitishwa makao makuu ya polisi Dar na wakurugenzi wenzake waliitwa na kuhojiwa akiwemo yeye mlalamikaji ,hata hivyo siku chache baada ya mahojiano hayo Saleh alipigiwa simu na kutakiwa kuripoti Takukuru Arusha"alisema wakili.
Wakili Rukaka alisema mteja wao alitii wito na kutinga Takukuru Arusha ,lakini hakupewa nafasi ya kujitetea wala kuambia kosa lake ila alielezwa kwamba hayo ni maelekezo kutoka ngazi za juu na kama anamalalamiko aandike barua.
"Mteja wetu aliamua kuandika barua ya malalamiko na nakala kwenda kwa DPP,DG,TAKUKURU, Katibu Mkuu Kiongozi, Jaji Kiongozi Mahakama ya Biashara Dar,NPS ARUSHA,ofisi ya DPP ARUSHA na katika barua zote hizo Mahakama pekee ndio walijibu kuwa tumepokea"alisema wakili Rukaka
Wakili alidai mteja wao alifungua kesi polisi dhidi ya wabia Wenzake, madai ambayo polisi Arusha hawakuyafanyiwa kazi badala yake yeye ndiyo aligeuziwa kibao na kukamatwa na Takukuru na baadaye kufikishwa mahakamani.
Hata hivyo taarifa zinadai kwamba wawekezaji hao wamekuwa na msuguano wa kibiashara baada ya Saleh kumwajiri Mtendaji wa kampuni hizo,Daudi Lumala (Eddy) na kwamba wabia wenzake wamekuwa wakimtaka Saleh ajitoe katika umiliki wa kampuni hizo ili wampatie hisa Eddy kama mtanzania aweze kusimamia kampuni hizo kwa sababu wao sio raia wa Tanzania jambo ambalo Saleh amegoma kuachia hisa zake.
Taarifa zaidi zinadai kwamba wawekezaji hao kutoka Saud Arabia wanapewa nguvu na mtoto wa kiongozi wa ngazi za juu pamoja na Mjumbe wa halmashauri kuu ya ccm M-NEC(Jina tunalo) jijini Dar es salaam.
Wakili Faisal anadai kwamba mteja wake analalamika kufunguliwa kesi mbili zinazofanana kesi ya madai mahakama ya biashara Dar na kesi ya Takukuru Arusha jambo ambalo wanahisi kuna maelekezo ya mtoto wa kigogo mwenye maslahi na wabia wenzake raia wa Saud Arabia.
Mshtakiwa wa pili Sheck Mfinanga ambaye yuko nje kwa dhamana anatetewa na Wakili Mariam mrutu na kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Octoba 24 mwaka huu katika mahakama ya Mkoa Arusha mbele ya Hakimu Mfawidhi Erasto Philly wa Mahakama ya hakimu Mkazi Arusha .
Mara ya mwisho kesi hiyo iliitwa mahakamani Octoba 10 mwaka huu na upande wa Mashtaka ambao unaongozwa na DPP haukuwepo mahakamani na wala haukutoa taarifa za udhuru wala kuleta taarifa yoyote ya kutokuhudhuria na hakimu aliahirisha shauri hilo hadi oktoba 24 Mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa
End....
0 Comments