Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, John Kayombo, ameibuka na majibu makali kufuatia madai yaliyotolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema, kuhusu dosari kadhaa katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwenye daftari la mkazi linaloendelea nchini.
Jana jumatatu Lema akizungumza na vyombo vya habari jijini hapa,alimshambulia vikali Mkurugenzi wa jiji la Arusha,John Kayombo akidai anatumika vibaya na ccm akidai ni mpango maalumu ulioandaliwa kumleta Arusha ili kuisaidia ccm kushinda katika uchaguzi huo jambo ambalo alisema amejipanga kula naye sahani moja labda ahamishwe.
"Watu wanasombwa kwa magari ya Haice kutoka kata moja kwenda kata nyingine kujiandikisha maana yake nini hii ni hujuma inayofanywa na msimamizi wa uchaguzi kwa kushirikiana na ccm"Alisema Lema!
Akizungumza ofisini kwake Kayombo ambaye pia ni msimamizi wa uchaguzi huo, amekanusha vikali madai ya Lema, akisisitiza kuwa zoezi la uandikishaji linaendelea vyema bila changamoto yoyote.
"Hakuna changamoto yeyote kwenye zoezi hili na ujue tuna vyama 19 vya siasa vilivyosajiliwa kamili, lakini ni chama kimoja tu kinacholalamika. Mjiulize shida iko kwa nani? Upande wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, hatuna shida kwenye zoezi hili. Tunakwenda vyema, na zoezi la uandikishaji litakwisha salama kabisa." Ameeleza.
Kayombo ameendelea kueleza kwamba zoezi la uandikishaji limefuata taratibu zote za kisheria na kwamba hakuna tatizo lolote lililoripotiwa.
"Sasa Lema anazungumza mambo ya nchi nzima, sisi hatuna mamlaka ya kujibu mambo ya nchi. Tunashughulika na zoezi hapa kwetu na hakuna shida yoyote. Kama wana shida, waje ofisini tuzungumze nao tujue, ila hadi sasa tunakwenda vyema na hakuna shida."
Pia, amesisitiza kuwa kila chama cha siasa kinatakiwa kufuata kanuni za uchaguzi wakati wa uandikishaji, badala ya kuendesha kampeni kabla ya wakati rasmi wa kampeni. "Tuhamasishe watu wajiandikishe, sio kuhamasisha huku unapiga nyimbo za vyama," ameeleza. Kayombo amesema ametoa maelekezo hayo kwa vyama vyote 19 vilivyosajiliwa nchini na siyo chama kimoja pekee.
Kuhusu madai ya baadhi ya mawakala kuzuiwa kuapishwa, Mkurugenzi huyo amesema hakuna jambo kama hilo, isipokuwa CHADEMA na viongozi wake wanapaswa kufahamu ni nani wa kuwaapisha na kwa wakati gani, kwa kurejea kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambazo zinaeleza kuwa kama chama kimekosa hakimu wa kuwaapisha mawakala wake basi Mkurugenzi ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi au wasaidizi wake watawaapisha badala ya hakimu.
“Hao CHADEMA sijawaona kwangu kwa lolote na mie siwezi kuwapigia simu kuwaita, ila hakuna shida yeyote ile kwenye uandikishaji hadi sasa”, amesema Kayombo na kuongeza kuwa hajawahi kumuona Lema ofisini kwake kuleta malalamiko yoyote,
"Mimi sijawahi kumwona ofisini kwangu akija kwa shida yeyote hadi sasa, ila namsikia huko mitandaoni tu akipiga kelele,"
Mapema jana siku ya Jumatatu, Godbless Lema alionesha kutoridhishwa na mwenendo wa zoezi hilo la uandikishaji. Amedai kuwa baadhi ya vituo vya uandikishaji havifanyi kazi kwa uadilifu na kwamba baadhi ya maafisa wa uandikishaji wanakwepa taratibu rasmi.
"Kuna kituo kimoja hapa Arusha, badala ya msimamizi anayeandikisha kuandika wanaoandikishwa kwenye daftari, anaandika kwenye karatasi ya pembeni," amesema Lema, akiongeza kuwa hali hiyo inatia mashaka kuhusu uadilifu wa zoezi zima.
Pia, Lema amebainisha kuwa kuna maelekezo ya kisiasa yanayolenga kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuwa mbaya, pengine kuliko ule wa mwaka 2019, huku akionya kuhusu hali ya wananchi kupoteza matumaini kwa mifumo ya uchaguzi na utawala wa kisiasa.
Aidha Lema alisisitiza kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa ni mchezo mchafu unaopangwa na ccm kwa kushirikisha vyombo vya dola ,usalama wa Taifa ili ccm iendelee kushika hatamu kwa kuwa na wenyeviti wa kutosha wa mitaa na vitongoji jambo ambalo alisema hatakubali kizembe!
Ends..
0 Comments