Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amewataka wananchi nchi nzima kufunga na kuwaombea mabaya viongozi wote wanaopanga na kushiriki kuhujumu utawala bora ikiwemo kuhujumu daftari la mpiga kura.
Aidha amewataka wachungaji na Maaskofu kutokaa kimya katika kukemea maovu kwa kuogopa kunyimwa mialiko ya serikali katika kusema ukweli juu ya mwenendo wa daftari la mpiga kura ambalo limejaa hila kwa kuandikishwa watoto wa shule,vichaa na marehemu.
ameyasema hayo leo ijumaa oktoba 25 , 2024 jijini Arusha wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na mwenendo wa daftari la mpigakura katika mikoa ya kanda ya Kaskazini, ambapo alisema katika mikoa hiyo na nchi nzima daftari limechezewa kwa kuandikishwa majina hewa ili kikinufaisha chama cha Mapinduzi.
"Tumefanya tathimini nchi nzima tumebaini udanganyifu mkubwa wa uandikishaji wa Daftari la mpiga kura,kwa mfano utakuta siku ya mwisho kituo kimoja watu walikuwa 175 lakini siku majina yamebandikwa utakuta yapo 600"Alisema Lema
Mwenyekiti huyo wa kanda ya Kaskazini alisema wao kama wapinzani hawatajitoa katika uchaguzi wa serikali za mitaa licha ya changamoto hizo ila aliwaomba wananchi kwa kila imani yao kuwaomba mabaya viongozi walioshiriki mpango huo mchafu wa kuchakachua majina daftari la mpiga kura.
"Huu udanganyifu wa uandikishaji sio wa Arusha pekee ama kanda ya Kaskazini bali ni nchi nzima tumeshuhudia clip inatembea mitandaoni watoto wa shule wakishangaa na kucheka kukuta majina yao yamebandikwa ukutani huku wakipewa umri wa miaka ya mtu mzima"
Lema alimtuhumu waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa kushiriki mpango huo mchafu wa kudhoofisha upinzani nchini kwa kuruhusu uandikishwaji wa wototo wenye umri mdogo na majina ya marehemu ili kuhujumu uchaguzi huo kwa lengo la kukipa ushindi chama cha Mapinduzi.
"Mchengerwa anajua kinachoendelea nchi nzima kuhusu idadi ya majina ya wapiga kura hewa na hachukui hatua yoyote kukemea udanganyifu huo ,mimi sina uwezo wa kumfanya chochote ila niwaombe wananchi kwa imani zao kufunga na kufanya maombi ya kuwalaani viongozi wote wanaoshiriki mchezo huo mchafu"
Katika hatua nyingine Lema alisema kuwa chama chake kimeweka magombea wote katika mitaa ya jimbo la Arusha mjini na majimbo ya mikoa ya kanda ya kaskazini na wanatarajia kuweka ushindani mkubwa ,japo alikiri kwamba baadhi ya wagombea wake wamevunjika moyo kutokana na uchakachuaji wa daftari la mpiga kura.
Ends..
0 Comments