Na Joseph Ngilisho ARUSHA
Mwekezaji Saleh aliyeketi, akijadiliana jambo na mawakiki wake ,Mosses Mahuna na Faisal Rukaka punde mara baada ya kesi kuahirishwa jana!
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya Uhujumu uchumi inayomkabili Mfanyabiashara na Mwekezaji Saleh Salim Alamry (54) na mwenzake wakili Sheck Mfinanga, kuharakisha upelelezi wa shauri hilo ili kesi ya msingi ianze kusikilizwa.
Hayo yameelezwa na Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo Erasto Philly baada ya wakili wa mashtaka Ahmed Mbagwa kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika ikiwa ni mara ya tatu kuieleza makamama hiyo kila washtakiwa wanapofikishwa mbele ya mahakama hiyo.
"Shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa kwa sababu upelelezi haujakamilika ila umefikia hatua nzuri ,tunaomba ahirisho wakati upelelezi ukiendelea"
Mawakili wa utetezi wa Saleh , Wakiongozwa na Moses Mahuna na Faisal Rukaka walipinga maelezo ya wakili Mbangwa na kuieleza mahakama kuwa mteja wake anateseka na mahakama inatumika kama kichaka cha kumtesa.
"Haiwezekeni kila mara upelelezi haujakamilika na mara ya mwisho upande wa mashtaka hawakufika mahakamani bila taarifa yoyote ni bora waiondoe kesi mahakamani na kumkamata tena na kumfikisha polisi kuliko kila.mara kudai upelelezi haujakamilika" .alisema Mahuna
Wakili Mahuna alidai mbele ya mahakama hiyo kwamba kuna haja gani ya kumkamata mteja wake na kumfikisha mahakamani na kumpa kesi ya uhujumu uchumi wakati wanajua hawana uhakika na mashtaka yao
"Unawezaji kumkamata mtu na kumpa makosa ya uhujumu uchumi unajuaje kama alitenda kosa hilo halafu unamfikisha mahakamani na kudai upelelezi bado hujakamilika"
"Hii inasikitisha na kutia aibu kwa maofisa wa serikali kuendelea na shauri bila kuwa na uhakika na makosa ya mshtakiwa na mahakama wanaitumia kama kichaka cha kumtesa mteja wetu"
"Naomba mahakama itoe amri ya kuwataka upande wa serikali kukamilisha upelelezi au waondoe mashtaka na wamkamate hapo nje ili wamfikishe polisi wakaanze upya"
Baada ya maelezo hayo Hakimu Philly alisema kuwa wakati unapomleta mshtakiwa mahakama na kushindwa kumsikiliz kwa wakati ni kumnyima uhuru na haki yake .
Mahakama hiyo imesisitiza pande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka ili kesi hiyo ianze kusikilizwa.
Hakimu Philly aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba saba mwaka huu na kuzitaka pande zote kufika kwa wakati mahakamani na mshtakiwa Saleh alirudishwa mahabusu gerezani na mshtakiwa wa pili Sheck Mfinanga akiendelea na dhamana yake .
Wakiongea nje ya mahakama mmoja ya ndugu wa mshtakiwa,Asma Salimu alimwomba jaji mkuu wa mahakama kuingilia kati ili mshtakiwa ambaye ni kala yake aweze kupata haki yake ya msingi kwa sababu kesi hiyo ni ya kupikwa kwa lengo la kumshurutisha kaka yake ajitoe kwenye kampuni za Sunset Tarangire limited na Alrajhi Holdings LTD wanazomiliki baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara na wawekez wenzake ambao wapo nje ya nchi nchini Saud Arabia.
Asma alisema ndugu wanashangazwa na mahakama kudai haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo wala kutoa amri zozote pasipo kupata hati au ruhusa ya Mwendesha mashtaka wa serikali DPP,lakini alitoa dhamana kwa mshtakiwa namba mbili ambaye pia anakabiliwa na shitaka hilo la uhujumu uchumi, Hivyo ameomba Jaji Mkuu kuingilia kati ili kaka yake apate dhamana.
"Kama mshtakiwa namba mbili ameachiwa na hakimu basi na ndugu yetu aachiwe kwa dhamana maana wote wanamakosa ya uhujumu uchumi ambayo kisharia hayana dhamana.
"kukaa ndani anapata hasara ambapo ameshindwa hata kuvuna mazao aliyowekeza ekari zaidi ya 2000 katika mashamba yake ambayo wamezuiwa na wabia wenzake ambao wanamgogoro wa uwekezaji".
Alizeti yote inazidi kuharibikia shambani,mifugo inaibwa kwa maana ndugu tumezuiwa na kwa kudaiwa ni maelekezo kutoka juu. Je hasara hii ya mamilioni mahakama au ofisi ya DPP watakubali kuilipa" Alilalamika Asma
Wakati huo huo Kesi ya madai iliyofunguliwa na Kampuni hizo tajwa dhidi ya Saleh katika Mahakama ya biashara divisheni ya Dar e salaam iliendelea jana mbele ya Jaji Dkt Cleophas Moris.
Kampuni hizo zinamdai Saleh zaidi ya dola za kimarekani milioni 26 ambazo walidai ni jumla ya gharama za hasara aliyowasababishia kwa kukosa uaminifu katika makampuni hayo, mchango wa mtaji katika makampuni yote, fedha za ukaguzi wa ndani pamoja na gharama za kesi.
Wakili wa Kampuni hizo ,Mnyiwala Mapembe aliomba mahakama kuliondoa shauri hilo bila gharama na kupewa ruhusa ya kulirejesha tena iwapo ataona inafaa
Wakili wa utetezi Faisal Rukaka anayemuwakilisha Saleh katika shauri hilo hakua na pingamizi la shauri hilo kuondolewa lakini aliomba mahakama gharama za kesi na wamejipanga kudai gharama za uendeshaji milioni 500.
Jaji Morris katika majumuisho na amri alikubali maombi ya kuondoa kesi na ruhusa ya kulirejesha kama wataona inafaa.
Ends...
0 Comments