KESI YA MAUAJI YA ASIMWE :PADRI KUPIMWA AKILI

By Ngilisho Tv- BUKOBA


Kesi ya mauaji ya mtoto Asimwe Novart, mwenye ualbino, aliyeripotiwa kutoweka nyumbani kwao Kamachumu mnamo Mei 30, 2024, na baadaye mwili wake kukutwa katika kalavati akiwa amekatwa viungo Juni 17, 2024, imeanza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba leo, Oktoba 25, 2024.

Watuhumiwa tisa wamefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kusomewa mashtaka yao na maelezo ya awali, baada ya mwenendo wa kesi kukamilika. 

Watuhumiwa hao wanahusisha Padri Elipidius Rwegoshora, ambaye ni mtuhumiwa namba moja, pamoja na Novat Venant – baba wa mtoto Asimwe, na wengine akiwemo Nurdin Ahmada, Ramadhan Selestine, Rwenyagira Alphonce, Dastan Buchard, Faswiu Athuman, Gozibert Arikad, na Dezdery Everigist.

Wakili wa utetezi, Projestus Mulokozi, aliyeteuliwa na Serikali, akiambatana na mawakili wengine wawili, aliwasilisha ombi kwa Mahakama kusitisha kwa muda kusomewa kwa mashtaka ya washitakiwa wote. 

Pia aliiomba mahakama imruhusu Padri Rwegoshora kufanyiwa uchunguzi wa afya ya akili kutokana na wasiwasi walioupata walipokuwa wakiongea naye.

Jaji Emmanuel Ngigwana alikubaliana na hoja hiyo na kuanza kumuuliza maswali mtuhumiwa huyo namba moja, Padri Rwegoshora, akisema,  

"Unajua kwa nini upo Mahakamani?"  

Padri alijibu, "Niliambiwa na RCO kuwa nimeua mtoto."Jaji alimuuliza tena,  

"Tangu umezaliwa, uliwahi kuwa na changamoto yoyote ya kiafya upande wa akili na ukapelekwa hospitali?"  

Padri alijibu, "Waga nina tatizo la kusahau na nilisimamishwa kazi eti maneno yangu sio mazuri."

Baada ya majibizano hayo, Jaji Ngigwana aliamua kesi hiyo haitoweza kuendelea hadi Padri Rwegoshora afanyiwe uchunguzi wa kina wa afya ya akili. 

Alitoa amri kwa mtuhumiwa huyo kupelekwa Isanga, taasisi maalum ya afya ya akili, kwa muda wa siku 42 kwa uchunguzi zaidi.

..Ends....

Post a Comment

0 Comments