JIMBO LA ARUSHA KUANZA KUANDIKISHA WAPIGA KURA KESHO IJUMAA OCTOBER 11,KAYOMBO AKAMILISHA MAANDALIZI KWA ASILIMIA 100,WANANCHI WATAKIWA KUJITOKEZA KWA WINGI ,ASIYEJIANDIKISHA HAKUNA KUPIGA KURA

Na Joseph Ngilisho, Arusha .

Jiji la Arusha limefungua pazia la wananchi wote wa jiji hilo   kujitokeza kwa wingi hapo kesho oktoba 11 kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura  kwa ajili ya kupata haki ya msingi ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,mwaka huu.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 11, mwaka huu ofisini kwake,Msimamizi wa uchaguzi,John Kayombo  alisema  kuwa ,maandalizi yote  yamekamilika na zoezi hilo la kuandikisha linatarajiwa kuanza mapema kesho oktoba 11  hadi oktoba 20 mwaka huu katika vituo vyote 462 ,kuanzia  saa 2  hadi saa 12 jioni. 


"Sisi katika halmashauri ya jiji la Arusha tumefanya maandalizi kwa asilimia 100 tumekamilisha maandalizi yote ya zoezi la uandikishaji na tumewakumbusha wadau wa uchaguzi ambao ni vyama vya siasa kuweka mawakala katika vituo vya uandikishaji na wahakikishe mawakala hao wameapishwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Wenyeviti wa mtaa na wajumbe wa kamati ya mtaa katika mamlaka za miji za mwaka 2024."alisema .


Alifafanua kuwa,mpaka sasa  kuna jumla ya vituo 462 vya kujiandikishia ambavyo vitasaidia  sana wananchi kutokaa  kwenye foleni kwa muda mrefu na kuondoa  msongamano   .

"Tuna vituo 462 tumeamua kuboresha kwa kuongeza vituo ili kusudi kutowafanya watu wasimame kwa muda mrefu kwenye vituo vya kujiandikisha na tutafanya hivyo na wakati wa kupiga kura ,tunaomba watu wote wajitokeze ,mtu ambaye hatajiandikisha ,hata pata fursa ya kupiga kura"


Aliongeza kuwa, tangazo la serikali namba 574 la mwaka 2024 nakala za viapo  zimetolewa  kwa viongozi wa vyama ili kuwarahisishia mchakato wa kuapisha mawakala .


Alifafanua kuwa ,orodha ya vituo vyote vya kujiandikisha kwa vyama vya siasa na.upangaji wa vituo umezingatia  azma ya kupunguza foleni ili kuruhusu watu kujiandikisha kwa wepesi na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji Mali.


Kayombo ambaye pia ni Mkurugenzi wa jiji la Arusha amewataka wananchi kutambua kuwa uchaguzi huu ni muhimu sana kwani wanakwenda kuchagua  viongozi watakaoshughulika  na mambo ya wananchi na maisha yao ya kila siku. 



"Nawaomba pia viongozi wa vyama vya siasa tuendelee kushirikiana katika hatua zote na endapo kiongozi yeyote wa chama atahisi kuna  changamoto yoyote katika zoezi la uandikishaji awasiliane na ofisi ya msimamizi wa uchaguzi."alisema


            

Ends...

Post a Comment

0 Comments